Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Ndugu Ramadhan Kailima akitangaza majina ya Madiwani wa Viti Maalum walioteuliwa na tume ya uchaguzi kutoka vyamba mbalimbali vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu nchini kote kutokana na idadi ya ushindi wa viti vya wabunge na madiwani kwa Chama husika.
Bw. Kailima ametanganza majina hayo wakati alipokutana na waandishi wa habari leo kwenye ofisi za Tume hiyo zilizopo jengo la Posta mkabala na Wizara ya Mambo ya Ndani.
…………………………………………………………………………..
NA SHAMIMU NYAKI- MAELEZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania ( NEC) leo imetangaza majina ya Madiwani wa viti maalum walioteuliwa na vyama vyao vya siasa kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Octoba 25 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Tume hiyo, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Tanzania Bw. Ramadhani Kailima amesema jumla ya viti maalum vilivyopo ni 1407 kutoka Kata 3923 cha Uchaguzi, ambapo viti 1393 ndivyo vilivyogawiwa kwa vyama vya siasa vilivyoshiriki Uchaguzi na kutimiza vigezo vya kupata Madiwani wa viti maalum.
Aidha katika mgawanyo huo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata viti 1,022 kikifatiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) viti 280 huku Chama Cha Wananchi CUF kikipata viti 79,ACT Wazalendo na NCCR-Mageuzi wakipata viti 6 kwa kila chama.
Ameongeza kuwa idadi kamili ya viti maalum itakamilika pale Uchaguzi katika Kata ambazo hazikufanya uchaguzi kukamilika na pia ameviagiza vyama vya siasa kukamilisha uwasilishaji wa majina ya waliowateuwa kuwakilisha Kata zao katika Uchaguzi Mkuu uliopita ili waweze kusajiliwa.
“ Waandishi muache malumbano ya mambo ya vyama vya siasa bali muhimize wananchi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi unaoendelea nchini ili kutimiza haki yao ya msingi ya kikatiba” alisema Bw Kailima.
Uchaguzi kwa majimbo ambayo hayakuweza kuwapata wawakilishi wao yanatarajiwa kufanya uchaguzi hivi karibuni. Majimbo hayo ni Lushoto, na Ulanga Mashariki ambao utafanyika tarehe 22 Novemba,mengine ni Ludewa na Masasi mjini utakaofanyika tarehe 20 Desemba na jimbo la Kijitoupele huko Zanzibar utafanyika hapo baadae.
Comments