Saturday, November 21, 2015

Jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere lakamilika asilimia 65


Jengo la tatu la abiria (TB III) linalojengwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam limekamilika kwa asilimia 65 na linavutia.
Jengo hilo lenye uwezo wa kuchukua abiria milioni 6 kwa mwaka limewavutia wahandisi ujenzi  kutoka mkoa wa Pwani waliolizuru leo na  wadau wa usafiri wa anga jana.
Akizungumza kwa niaba ya Wahandisi wenzake leo, Mhandisi Michael Mrema amesema, mradi huo ni mkubwa, mzuri na wenye tija kwa uchumi wa nchi na kwamba wamefurahi kupata nafasi ya kujifunza ulivyo.
Meneja Mradi wa Bam International ya Uholanzi inayojenga jengo hilo, Eric Van Zuthem amesema leo, wamefurahi kupata fursa ya kuwajengea Watanzania hasa wadau wa usafiri wa anga jengo hilo la aina yake.
“Jengo hili litakuwa la kimataifa kutokana na vifaa vya usalama vitakavyofungwa hasa ukizingatia hivi sasa kuna matukio ya ugaidi kama yaliyotokea Ufaransa karibuni. Ni furaha kufanya kazi na TAA na wadau pia kuwajengea Watanzania, jengo zuri litakalovutia wageni.’ amesema.
Mkurugenzi wa Mradi wa TB III, Mhandisi Mohammed Millanga amesema, mradi huo unaotekelezwa kwa awamu mbili, utakamilika mwaka 2017. Amesema awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Juni 2016.
Amewaeleza Wahandisi hao kuwa Mkandarasi, Bam International alipewa zabuni moja ya kujenga kwa awamu mbili ambapo awamu ya pili inatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya Serikali kuridhia kutolewa fedha.
Amewaeleza wahandisi hao jengo hilo linajengwa kwa gharama ya Euro milioni 235 (sh. Bilioni 518). Awamu ya kwanza inagharimu Euro milioni 133.2 (sh. Bilioni 293) na ile ya pili itagharimu Euro milioni 102 (sh. Bilioni 225).Kati ya fedha hizo, asilimia 85 inagharamiwa na Benki ya HBSC ya Uingereza kupitia mkopo unaodhaminiwa na Serikali ya Uholanzi na asilimia 15 Benki ya CRDB za mkopo unaodhaminiwa na Serikali ya Tanzania. Tayari Uholanzi imetoa fedha za awamu ya pili ili kazi ianze.
Mbali ya kuchukua abiria milioni 6, jengo hilo litakuwa na miundombinu ya madaraja makubwa ya abiria matano ya kuegesha ndege 18 na ndege moja kubwa aina ya  Airbus 380. Pia litakuwa na migahawa, sehemu za kusali, watoto kucheza na theluthi moja yake  ni sehemu za biashara.
Jana wadau kutoka mashirika ya ndege, wauza tiketi za ndege, wauzaji vifaa vya ujenzi, mawakala wa mizigo ikiwemo Swissport, maofisa ubalozi walizuru jengo hilo na kusifu ubora wake, miundombinu na viwango vyake.
Kutokana na abiria wanaotarajiwa kuongezeka baada ya jengo hilo kukamilika, Mhandisi Millanga amesema TAA inafikiria kuongeza njia za kurukia ndege ziwe mbili ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la ndege zirukazo JNIA.

Amesema TAA inafikiria kuongeza njia hiyo ili moja itumiwe na ndege ndogo tu na nyingine kubwa. Kwa sasa JNIA ina njia moja ya kurukia ndege na abiria wanaopita jengo la pili la abiria, wanakadiriwa kuwa milioni 2.5. 
Sehemu ya mbele
Sehemu ya  nyuma
Ubavuni

No comments: