Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Uongozi wa Mtandao wa Wanawake Tanzania (WFT) wakati viongozi hao walipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam,leo Nov 24, 2015 kwa mazungumzo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipokea baadhi ya Vipeperushi na Vitabu vya Mtandano wa Wanawake Tanzania (WFT) kutoka kwa mwenyekiti wa mtandao huo, Prof.Ruth Meena, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dares Salaam, leo Nov 24, 2015.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mtandao wa Wanawake Tanzania (WFT) baada ya mazungumzo yao yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dares Salaam, leo Nov 24, 2015.
Picha na OMR
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na uongozi wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania (WFT) ambapo amezungumzia dhamira ya serikali katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo mbali mbali yanayowakabili wanawake na watoto wa kike nchini.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais aliueleza ujumbe huo kuwa wakati wa kampeni aliahidi pamoja na kazi za kumsaidia Mhe. Rais bado kama mama atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi ya kupatikana kwa maji safi na salama, kuboresha afya ya mama na mtoto, elimu na mazingira.
“Nilipokuwa kwenye kampeni nimejionea shida ya maji na wanawake ndiyo wanaopata tabu ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji. Kwa hiyo, pamoja na kazi zangu za kumsaidia Mhe. Rais nitasimamia miradi yote ya maji, alau tuhakikishe maji yanapatikana umbali wa mita 400 kutoka eneo wananchi wanakoishi au karibu zaidi”.
Alisema kinachofurahisha zaidi suala la maji liko kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na miradi mingi ikiwemo ya kuchimba visima virefu katika mikoa kama vile ya Singida na Dodoma iko kwenye mchakato na cha msingi ni kusimamia fedha zinatumika kuleta maji kama ilivyokusudiwa.
Kuhusu afya ya mama na mtoto alisema kazi hiyo ataianza hivi karibuni kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za wanawake ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mimba za utotoni.
“Hili tutajitahidi kulipunguza kwa kiasi kikubwa na hasa baada ya serikali ya Awamu ya Nne kusema kwamba shule ya msingi ya lazima ni kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha nne”, alisema na kuongeza
“Katika kipindi hicho binti atakuwa amefikisha miaka 17, atakuwa tayari kukabiliana na mambo ya uzazi tofauti na ilivyo sasa ambapo anamaliza darasa la akiwa mdogo na matokeo yake anapata mimba katika umri mdogo. Mtusaidie kupiga debe huko nje utekelezaji uweze kufanikiwa.”
Hata hivyo, alisisitiza kusimamia suala la kuhakikisha zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini zinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha katika wodi za wazazi kwa ajili ya kuhudumia akina mama na wananchi kwa ujumla ambao wengi wanaonekana ni watiifu kwa serikali yao.
Kwa upande wa elimu Mhe. Samia alisema atasimamia ujenzi wa mabweni kwa watoto wa kike na kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa sababu uharibifu wa mazingira ndiyo umekuwa chanzo cha upungufu wa maji nchini.
Aidha aliuambia ujumbe huo kuwa hivi sasa tuna mpango wa kuimarisha utendaji serikalini kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa ili kinachopatikana kidogo kimfikie kila mwananchi.
“Tutaendelea kuaihirisha sherehe ili fedha hizo ziweze kutumika kwa mambo ya kijamii. Kwa msimamo huu amabao Mhe. Rais ameanza nao labda watu wote tushirikiane kwa kutatua matatizo yetu kwa gharama nafuu kwa ufanisi mkubwa.”
Mapema akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Mtandao huo Prof Ruth Meena alimpongeza Mhe. Samia kwa kushika nafasi ya juu ya uongozi akiwa mwanamke wa kwanza kuweka historia katika Tanzania.
Alimweleza Mhe. Makamu wa Rais matarajio yao kwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa itatetea misingi ya haki na usawa katika Nyanja zote.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
24/11/2015.
Comments