TAARIFA YA KAIMU MKURUGENZI WA UCHAGUZI TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI KUHUSU UPIGAJI KURA KATIKA UCHAGUZI UTAKAOFANYIKA KATIKA MAJIMBO MAWILI NA KATA SITA


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa taarifa kuhusu upigaji kura katika uchaguzi utakaofanyika kesho tarehe 22 Novemba, 2015 katika majimbo mawili na kata sita ambapo uchaguzi wake ulihairishwa.
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume ya Taifa ya uchaguzi Bwa. Emmanuel Kawishe amesema kuwa Tume ilitoa taarifa kwa kuhairishwa kwa Uchaguzi katika Jimbo ya Lushoto mkoani Tanga, Jimbo la Ulanga Mashariki mkoani Morogoro, kata ya Muleba, Uyole, Bukene, Msingi, Bomang’ombe pamoja na kata ya kasulo kutokana na vifo vya wagombea.
“Kesho ni siku ya kupiga kura ya kuchagua Mbunge katika majimbo mawili na kuchagua Diwani katika kata sita, natoa rai kwa wale wote mliojiandikisha kama wapiga kura katika majimbo na kata hizo kujitokeza kwenye vituo mlikojiandikisha ili kuweza kupiga kura na kuwachagua viongozi mnaowataka bila hofu, woga wasiwasi au ushawishi” aliongeza Kaimu Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo Bwa. Kawishe alisema kuwa vituo vitafunguliwa kuanzia saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi jioni  na kuwakumbusha wapiga kura kubeba kadi yake ya mpiga kura.
“Kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga na wazee ambao hawatatakiwa kujipanga kwenye foleni”
“Wakati wote wa kupiga kura na kuhesabu kura, mawakala wa vyama vya siasa wawepo kwenye vituo na wajibu wao ni kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea hivyo hawatakiwi kuingilia masuala ya utendaji ambayo yamekabidhiwa kwa msimamizi wa kituo” alifafanua Bwa. Kawishe.
 Mbali na hayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewapongeza wananchi kutoka majimbo na kata zinazofanya uchaguzi kesho kwa uvumilivu waliouonyesha katika kipindi chote cha kusubiri siku ya kupiga kura kumchagua Mbunge au Diwani wao.

Comments