TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Agizo alilolitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge zipelekwe Katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda na magodoro ya wagonjwa wanaolala chini limetekelezwa.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema fedha hizo zimefanikisha kupatikana vitanda 300 vya wagonjwa pamoja na magodoro yake, shuka 600, Baiskeli za kubebea wagonjwa na vifaa vingine na kwamba hivyo vyote tayari vimepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Balozi Sefue ameuagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha vitanda vyote vinafungwa leo Jumapili na kwamba atakwenda kuvikagua siku ya kesho, Jumatatu vikiwa tayari vinatumiwa na wagonjwa waliokua wanakosa vitanda vya kulalia na kulazimika kulala chini.
Wadau mbalimbali walichanga fedha kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge baada ya uzinduzi rasmi wa bunge la 11 lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliagiza fedha hizo zitumiwe kwa kiasi kidogo kisichozidi shilingi milioni 15 na nyingine zipelekwe hospitali ya Muhimbili kutatua tatizo la uhaba wa vitanda.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU,
Novemba 21, 2015
Comments