Katibu wa klabu ya Gofu ya Lugalo Kanali Mstaafu John Nyalusi akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam juu ya mashindano ya siku moja ya gofu ya kumuenzi Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara yatakayofanyika katika klabu ya Gofu ya Lugalo jumamosi hii. Kulia ni Meneja chapa (vileo vikali) wa Serengeti Breweries Limited, Shomari Shija ambao wanahusika na udhamini wa utoaji tuzo, vinywaji na burudani katika kipindi chote cha mashindano.
Meneja chapa (vileo kali) wa Serengeti Breweries Limited, Shomari Shija, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuhusiana na mashindano ya siku moja ya gofu ya kumuenzi Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara yatakayofanyika katika klabu ya Gofu ya Lugalo jumamosi. Kushoto ni katibu wa klabu ya Gofu ya Lugalo Kanali Mstaafu John Nyalusi. Kampuni ya bia ya Serengeti kupitia kinywaji chake kikali cha Johnnie Walker kitadhamini mashindano na kutoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa mchuano huo.
Mabalozi wa pombe kali ya Scotch Whisky “Johnnie Walker” wakionyesha aina mbalimbali za chapa za pombe hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari juu ya mashindano ya gofu ya waitara ambayo yanatarajiwa kuanza rasmi siku ya jumamosi katika viwanja vya Lugalo jijini Dar es salaam. Kampuni ya bia ya Serengeti kupitia pombe hiyo kali ndio wadhamini wa mashindano hayo ambapo pia watahusika na utoaji tuzo, vinywaji na burudani katika kipindi chote cha mashindano.
KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) kupitia pombe yake kali ya Johnnie Walker imetangaza rasmi udhamini wa mashindano ya gofu ya Waitara ambayo yanatarajiwa kuanza siku ya jumamosi katika viwanja vya jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja hivyo, Meneja Chapa wa pombe wa Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) Bw. Shomari Shija alisema kuwa udhamini wa mchezo huu wa gofu ni kuhakikisha kuwa unaweza kuendelea na kusifika kama michezo mingine ikiwa pia kama moja ya sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii inayotuzunguka.
“SBL inadhamini michuano hii kwa kipindi cha miaka mitano sasa na itajikita hasa katika udhamini wa utoaji wa tuzo, vinywaji na burudani katika kipindi chote cha mashindano”…alisema Bw. Shomari.
Naye katibu wa michuano hiyo ya gofu Kanali mstaafu John Nyalusi aliishukuru SBL kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya mchezo huo na kuyaomba makampuni mengine kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizo za kuinua mchezo wa gofu nchini.
“SBL imekuwa katika mstari wa mbele katika kuuendeleza mchezo wa gofu nchini. Ni moja kati ya wadhamini wetu wa kudumu kwa sasa…hivyo tunawashukuru sana… tunaomba makampuni mengine zaidi yajitokeze kuunga mkono jitihada hizi,” alisema Kanali Nyalusi.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kufunguliwa na jaji mstaafu Ndugu Mark Bomani siku ya jumamosi saa nne asubuhi na kuwa mpaka sasa mwitikio umekua mkubwa na tayari wachezaji 150 wameahidi kushiriki mashindano hayo kutoka vilabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wenyeji wa Lugalo Golf club, Dar es salaam Gymkhana club, Morogoro Gymkhana club, Arusha n.k.
Mashindano ya gofu ya Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali George Waitara huandaliwa na kufanyika kila mwaka kwa madhumuni ya kuenzi mchango wake wa kimichezo nchini kwa kuasisi uwanja wa gofu wa Lugalo golf club. Uwanja wa gofu wa Lugalo ulianzishwa mwaka 2006 kwa mchango mkubwa uliotolewa na Generali mstaafu George Waitara kipindi alichokuwapo madarakani, pia kuendelezwa na Mkuu wa Majeshi aliyefuata na aliyeko madarakani kwa sasa Generali Davis Mwamunyange.
Comments