Friday, August 14, 2015

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA SHINYANGA, KHAMISI MGEJA NA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA CCM DAR ES SALAAM, JOHN GUNINITA WAJITOA CCM NA KUJIUNGA CHADEMA

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamisi Mgeja. jana Agosti 13, 2015, alitangaza kujivua wadhifa huo na kukihama chama chake na kujiunga na CHADEMA

NA K-VIS MEDIA
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi , CCM, Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja jana Agosti 13, 2015, alitangaza kujivua wadhifa huo na kukihama chama hicho na kujiunga na chama cha upinzani CHADEMA.
Pia aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John John Guninita, naye amekihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Wote Hao walitoa msimamo huo mpya wakati wakiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Wimbi la viongozi wa CCM kukihama chama hicho limeendelea kukua baada ya aliyekuwa Mbunge wa Sikonge kupitia chama hicho, Said Nkumba, naye kutangaza kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Sababu za viongozi hao kukihama chama chao, karibu zinafanana, wamedai kuwa wamechukua uamuzi huo baada ya kubaini CCM imepoteza mwelekeo na kwamba kinaendeshwa kibabe tofauti na misingi ya kuasisiwa kwake.
Vingozi wengine wa juu wa CCM, waliokwishatangaza kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA, ukiacha waziri Mkuu wa zamani Mh. Edward Lowassa, ambaye sasa ni mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, akiwakilisha vyama vinavyounda UKAWA, ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, aliyewahi kuwa mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, naibu waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Milton Makongoro Mahanga, aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli, na aliyekuwa
Mbunge wa Viti Malum, Esther Bulaya. Hali kadhalika madiwani kadhaa kutoka mkoani Arusha wamekwishatangaza kukihama chama hicho.
Post a Comment