Wednesday, August 26, 2015

SERIKALI YASAINI MKATABA WA ZAIDI YA SH. BILIONI 422 KUIMARISHA SEKTA YA AFYA NCHINI.

1
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kushoto) akisaini hati ya makubaliano ya mkopo nafuu kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ili kuimarisha sekta ya afya nchini katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi Bella Bird.
2
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kushoto) akibadilishana hati ya makubaliano ya mkopo nafuu na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi Bella Bird (kulia) mara baada ya kusaini hati hiyo ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ili kuimarisha sekta ya afya nchini leo jijini Dar es salaam.
3
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini hati ya makubaliano kuimarisha sekta ya afya nchini leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi Bella Bird.
4
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi Bella Bird (kulia) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini hati ya makubaliano kuimarisha sekta ya afya nchini leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile.
5
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Deo Mtasiwa (kulia) akisisitiza jambo wakati hafla ya usatiji saini hati ya makubaliano kuimarisha sekta ya afya nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia leo jijini Dar es salaam.
6
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango na Sera Bernard Konga (kulia) akitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kwa kuthamini sekta ya afya leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Deo Mtasiwa.
8
Baadhi ya waandishi wa habari na viongozi wa serikali na wawakilishi wa Benki ya Dunia waliohudhuria hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya mkopo nafuu kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia katika kuimarisha sekta ya afya nchini leo jijini Dar es salaam.
(Picha Eleuteri Mangi-MAELEZO)
………………………………………………………………………………………..
Na Allen Mhina –MAELEZO
Serikali kupitia mpango wa kuimarisha afya duniani, imepokea Dola za Kimarekani milioni 200 sawa na Sh. Bilioni 422.8 toka Benki ya Dunia ili kuimarisha sekta ya afya nchini. 
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile wakati wa hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya mpango wa kuimarisha sekta ya afya nchini iliofanyika leo jijini Dar es salaam kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia. 
Akiongea na waandishi wa habari na baadhi ya viongozi wa serikali na wawakilishi wa Benki ya Dunia, Dkt. Likwelile alisema kuwa dhumuni la makubaliano ya mpango huo ni kuwezesha na kuimarisha sekta ya afya na vitendea kazi vitakavyowezesha uzazi salama kwa wakina mama wakati wakujifungua na kupunguza idadi ya vifo vya watoto kutokana na mapungufu wa afya bora.
Dkt. Liwalile, aliongeza kuwa kuna umuhimu na makusudio ya dhati kuimarisha sekta hiyo kutokana na uwepo wa vifo vinavyozuilika kwa wakina mama na watoto, kama inavyodhihirisha takwimu zilizotolewa wizara ya afya kuonesha kuwa kuna kuna idadi kubwa ya watoto wanaofariki wakati wa uzazi kwa kukosekana kwa vitendea kazi na huduma bora wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi Bella Bird ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuonesha juhudi za dhati kutekeleza mpango huo.
Bi Bella amesema kuwa amefurahishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kusimamia sekta ya afya ambapo alitembelea baadhi ya vituo wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani na kujionea hali ilivyo na kuhaidi kushirikiana vizuri na serikali ili kukamilisha mpango huo na kuleta mabadiliko katika sekta ya afya nchini.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bernard Konga aliishukuru Serikali na Benki ya Dunia kwa kuthamini sekta ya afya na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika kuendeleza sekta ya afya kama ilivyokusudiwa na ili kuboresha sekta ya afya ya kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya taifa kwa ujumla.

No comments: