JESHI LA POLISI KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM LAPIGA MARUFUKU WAGOMBEA WA VYAMA VYA SIASA KU FANYA VITENDO VINAVYOHATARISHA USALAMA.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE
25/08/2015
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limegundua kwamba kuna baadhi ya wagombea wa vyama vya siasa ambao wameanziasha mtindo wa kutembelea maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kama vile vituo vya daladala, masoko mbalimbali, n.k. kwa madai ya kuyatembelea makundi ya watu wenye kipato cha hali ya chini.
Kutokana na uzoefu uliojitokeza katika ziara hizo zisizo rasmi ni kwamba imeonekana mikusanyiko mikubwa isiyotegemewa katika hali ambayo inaashiria uvunjivu wa amani. Wakati wa ziara za aina hiyo yamejitokeza makundi ya watu mbalimbali kama vile waendesha bodaboda, machinga na makundi mengine katika namna ambayo imeleta taharuki pamoja na usumbufu unaotokana na makele, msongamano au shughuli za usafiri kusimama kabisa.
Tarehe 25/08/2015 majira ya saa 12:00 mchana katika makutano ya mtaa wa SWAHILI na UHURU Kamnda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala Kamishna Msaidizi Mwandamizi LUCAS MKONDYA alilazimika kukutana ana kwa ana na mgombea urais wa CHADEMA Mhe. EDWARD LOWASA ili kumpa tahadhali hiyo ya kiusalama. Mgombea huyo alikuwa amezungukwa na wapanda pikipiki wasiopungua arobaini pamoja na magari mengi katika hali ambayo ilileta msongamano katika eneo hilo ya barabara za Swahili na Uhuru. Msongamano huo ulileta athari na malalamiko kutoka kwa watumiaji wengine wa barabara jijini Dar es Salaam.
Aidha, imegundulika kwamba mgombea huyo alianzia kuzunguka maeneo mbalimbali ya Temeke kuanzia tarehe 24/08/2015 akitumia vyombo mbalibali vya usafiri ikiwemo mabasi ya abiria.
Ni lazima ieleweke wazi kwamba moja ya kazi za Jeshi la Polisi ni kuthibiti makundi makubwa ya watu katika namna ambayo kiongozi yeyote wa aina ya wagombea urais anatakiwa kulindwa katika kipindi chote cha kampeni hadi siku ya uchaguzi n.k. Ni vyema wagombea mbalimbali hususani wagombea urais waonyeshe ushirikiano wa hali ya juu kwa Jeshi la Polisi ili kuzuia madhara ya aina yoyote dhidi yao. Hivyo, ni muhimu wakajihadhari kwenda katika makundi yasiyo rasmi kwa sababu za kiusalama.
Tunawashauri viongozi wa vyama pamoja na wagombea wao wafuate ratiba za kampeni za mgombea urais/mgombea mwenza kwa vyama vya siasa kama ilivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuondoa hisia za kufanyika kampeni nje ya ratiba.
S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
DAR ES SALAAM
Comments