Friday, August 21, 2015

MIAKA 10 YA UKUWAJI WA SEKTA YA MAWASILIANO, TANZANIA

download (21)

Na Semu Mwakyanjala, TCRA
KUMEKUWEPO na ukuaji  mkubwa na mpana wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania kwa upande wa miundombinu na huduma ambavo kwa pamoja vimeleta faida kwa Watanzania  katika miaka ya hivi karibuni. Sekta hii inaongozwa na Sera ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA) ya mwaka 2003.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kwa kifupi TCRA, ni chombo huru cha Serikali kinachohusika na kusimamia sekta ya mawasiliano na utangazaji nchini Tanzania na ina majukumu ya kutoa   leseni kwa makampuni ya mawasiliano, ikiwemo ya huduma za simu, utangazaji, intaneti na posta na usafirishaji wa vifurushi.
TCRA ilianzishwa chini ya Sheria ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania Na 12 ya 2003 ambayo iliziunganisha zilizokuwa Tume ya Utangazaji Tanzania na Tume ya Mawasiliano Tanzania. Tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake 1 Novemba 2003, TCRA iomekuwa ikiwashirikisha wadau wake muhimu kupitia mashauriano kwenye masuala mbalimbali.
Ukuaji imara na wa kasi wasekta ya mawasiliano nchini ni sehemu ya matunda yanayoonekana na Serikali ya  Awamu ya Nne ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Sera nzuri za serikali na kufunguliwa kwa soko huria zimewezesha kuongezeka kwa wawekezaji na hivyo kuwapa watumiaji fursa ya kuchagua huduma bora wanayohitaji kwa gharama wanazomudu.
Kuanzishwa kwa mfumo wa leseni za muingiliano yaani (Convergence Licencing Framework) ambao ulianzishwa mwaka 2005 kutokana na kuendelea kukua kwa kasi kwa teknolojia kulikopelekea mwingiliano wa Teknolojia (Technological Convergence) kumechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa sekta ya mawasiliano.
Mfumo huu una aina nne za leseni ambazo ni:
  • Leseni ya Mitandao (Network Facility):
          Inajumuisha miundombinu ya setelaiti, mitandao inayotumia waya aina ya optic fibre, uwekaji wa nyaya na njia za mawasiliano, vifaa vya mawasiliano kutumia redio, milingoti ya mawasiliano ya simu za mkononi, minara na vifaa vya kurushia matangazo ya vyombo vya utangazaji;
  • Leseni ya Mtandao wa Simu (Network Services):
          Hii ni leseni inayoruhusu kutoa huduma za simu yaani sauti, picha na takwimu (voice, data, etc);
  • Leseni ya Huduma (Application Services):
          Hii ni leseni inayoruhusu mmiliki kutoa huduma kama vile internet, kupiga simu kupitia internet, takwimu kwa ajili ya biashara, na huduma za kutuma taarifa fupi;
  • Leseni ya Huduma ya Maudhui ( Content Services):
          Hii ni leseni inayoruhusu mmiliki kutoa huduma za utangazaji  wa redio na televisheni na taarifa kupitia mitandao ( online publishing) na taarifa za habari.
Leseni chini ya mfumo wa  CLF zinatolewa kwa ajili ya kutoa huduma katika ngazi nne- ngazio ya kimataifa, ya kitaifa, ya mkoa na wilaya.
Maendeleo tunayoshuhudia kwenye sekta ya mawasiliano nchini ni sehemu ya  matokeo ya mpango mkakati wa  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wa 2006/7 hadi 2010/11 na 2011/12 hadi 2015/16 ambao ulibuniwa na kutekelezwa Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi na kuwezeshwa na kuchangiwa na juhudi  za watumishi wa Mamlaka ambao wanafanya kazi kwa bidii na weledi.
TCRA inatekeleza mpango mkakati  sambamba na dira,dhima au dhamira na lengo kuu la Mamlaka.
Dira ya TCRA ni  “Kuwa Mdhibiti mwenye hadhi ya kimataifa, kwa kuweka na kusimamia usawa katika haki na majukumu ya watoa huduma za mawasiliano na kuendeleza huduma zinazojali mazingira, na uwezo wa kiuchumi wa watumiaji.”
Dhima au dhamira ya Mamlaka ni   “Kuwa na mfumo mahsusi wa usimamizi, kuboresha utendaji wa watoa huduma, na kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kwa lengo la kutoa mchango wetu kwa uchumi jamii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
Lengo kuu ni”  Kuendeleza ustawi wa Watanzania kupitia mfumo wa usimamizi wenye ufanisi na ambao unawezesha kupatikana kwa huduma za mawasiliano kwa wote”.
Soko la TEHAMA  limekuwa kwa idadi ya watumiaji wa huduma hizo, kwa aina mbalimbali za huduma hizo na kwa kuongezeka kwa eneo ambamo huduma mbalimbali zinapatikana; ingawaje idadi ya watumiaji wa simu za mezani imepungua. Kuna laini za simu za mkononi zipatazo 31,862,656 sasa ukilinganisha na laini 2,963,737 mwaka 2005.  Watumiaji wa intaneti wameongezake hadi kufikia 11,000,000 Desemba 2014 kutoka 3,563,732 mwaka 2008. Kwa sasa, kuna hamu kubwa ya matumizi ya intaneti na mwelekeo huu utaendelea; hasa kutakapokuwa na ongezeko la mitandao inayowezesha kutoa huduma za intaneti; na kuongezeka kwa mitandao ya jamii.
Sekta ya mawasiliano ni mojawapo ya sekta zinazoajiri watu wengi zaidi. Matumizi a simu za mkononi yamebadilisha mfumo wa maisha ya wananchi hapa nchini. Simu za mkononi siio tu kifaa cha mawasiliano 9 kwa kuongea na kutuma ujumbe mfupi au meseji0 lakini pia ni chombo cha kuimarisha watumiaji kiuchumi. Simu za mkononi zina matumizi ya aina mbalimbali ya kijitali kama vile huduma za fedha ambazo zinawawezesha watu kutuma na kupokea pesa. Watumaji wa huduma za fedha kuopitia simu za mkononi hivi sasa wanaweza kununua umeme, kulipia maji na kulipia huduma nyingine bila ya kuzalimika kwenda nje ya nyumba zao.
Watumiaji wanaweza kutoa pesa kwenye mashine za benki (ATM) na watu wengine wamejikomboa kutokana na adha ya kukaa foleni ndefu na kupoteza  muda ambao wangeutumia chini ya mfumo wa zamani wa kibenki.
Post a Comment