KILOMETA 6,276 ZA BARABARA ZAJENGWA NCHINI KWA MIAKA 10

Wakati wakandarasi walipokuwa wanajenga daraja hili katika eneo la Miangalua kwenye barabara ya Tunduma-Sumbawanga mwaka 2011. Barabara hiyo sasa imekamilika.
Barabara ya Mwanza-Musoma iko katika hali nzuri. 
(Picha zote na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).
………………………………………………………………………………………………..
 Na Daniel Mbega, brotherdannyblog
Sumbawanga: NAJIWEKA vyema kwenye kiti na kutazama nje kupitia dirishani. Japokuwa giza limetanda majira haya ya saa 4:30 usiku, lakini ninaweza kuhisi jinsi basi hili nililopanda la kampuni ya Majinjah linavyotafuna lami.
Abiria mwenzangu wa jirani ananiambai tutaingia saa sita kasoro usiku mjini Sumbawanga mjini. Nafarijika japo uchovu ni mwingi, maana kuketi kwenye basi kwa saa takriban 15 siyo mchezo ingawa tulipata nafasi mara kadhaa za kupumzika ‘kuchimba dawa’ na kupata mlo.
“Barabara yote ni lami tupu ndugu yangu, kasoro tu ni haya matuta kutoka Tunduma hadi Sumbawanga, lakini yamesaidia kupunguza mwendokasi,” ananieleza.
Tunduma tumeondoka kama saa tatu hivi kuzikabili kilometa 222 hadi Sumbawanga, lakini safari hii ya kutoka Dar es Salaam inayokadiriwa kuwa na umbali wa kilometa 1,000 imekuwa siyo ndefu licha ya uchovu wa kiuno na mgongo kutokana na kuketi tangu saa 12 alfajiri. Faraja pekee ni kwamba ninatumia siku moja tu kufika Sumbawanga, tofauti na miaka mitano iliyopita ambapo nililazimika kutumia siku mbili huku nikiingia gharama za ziada za kulala Lodge pale Mbeya kutokana na kutokuwepo na usafiri wa uhakika kutokana na ubovu wa barabara.
Wakati huo, ukilala Mbeya unalazimika tena kuamka mapema kuwahi basi ambalo licha ya kuondoka saa 12 alfajiri, bado litafika Sumbawanga saa 8 mchana.
Jirani yangu ananiambia kwamba sasa unaweza kwenda na kurudi Sumbawanga mara mbili ukitokea Mbeya kwani mabasi ni mengi na njia ‘inateleza’.
“Wametukomboa sana, magari hayajazi kama zamani, unasafiri kwa raha na kwa wakati – muda wowote unaotaka,” ananieleza.
Ndiyo. Nakumbuka safari moja wakati nikitokea Sumbawanga jinsi basi lilivyokuwa limejaza abiria mpaka sehemu ya kupita ikakosekana. Walioketi walikuwa wachache kuliko waliosimama, sasa piga hesabu lilikuwa na abiria wangapi! Hata kondatka mwenyewe alilazimika kupita kwa kuinama juu ya siti ili kwenda nyuma kuwapanga abiria waliosimama na kuchukua nauli. Ilikuwa ni hatari.
Lakini leo barabara hii imetandikwa lami na imekuwa sehemu ya barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 6,276 ambazo zimetengenezwa na utawala huu wa Awamu ya Nne, huku sehemu kubwa yabarabara hizo ikiwa imesimamiwa na Dk. John Pombe Joseph Magufuli kama Waziri wa Miundombinu.
Nimezunguka karibu nchi nzima nikifanya habari za uchunguzi kwa miaka kumi iliyopita. Mazingira ya wakati ule na ya sasa ni tofauti kabisa, maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki, hivi sasa hali ni nzuri. 
Tangu Januari hadi Juni 2015 pekee nimezunguka karibu kilometa 20,000 hapa nchini. Nimezunguka nikitokea Iringa kwenda Arusha kupitia Dodoma-Singida hadi Manyara; nimezunguka kutoka Dar es Salaam-Kiteto-Kondoa hadi Babati; nimepita Babati-Kondoa-Mayamaya hadi Dodoma; nimepita Mwanza-Shinyanga-Tabora-Mpanda hadi Sumbawanga mpaka Mbeya; nimetoka Dar es Salaam-Njombe-Songea hadi Mbambabay; nimetoka Mwanza-Musoma hadi Sirari; nimezunguka Mwanza-Sengerema-Geita hadi Bukoba; nimetoka Bukoba kupita Kahama hadi Dar es Salaam; nimetoka Shinyanga-Maswa-Bariadi hadi Lamadi; na maeneo mengine mengi kwa miezi sita.
Hakika nilichokiona kinastahili kupongezwa kwamba kimefanyika. Ingawa barabara kadhaa zimesimama kutokana na kukosekana kwa fedha kufuatia msukosuko wa wafadhili kushindwa kutoa fungu, lakini nyingi kati ya hizo zimekamilika na kuiunganisha vyema Tanzania.
Nilipita wakati fulani ilipoanza kutengenezwa barabara hii, nadhani ilikuwa mwaka 2011 nikiwa katika harakati zangu za kuandika habari za maendeleo vijijini. Barabara hii ilimegwa katika vipande vitatu ili kuharakisha ujenzi wake na kuzingatia ubora.
Kipande cha kwanza kilikuwa kutoka Tunduma hadi Ikana chenye urefu wa kilometa 63.2 ambacho kilijengwa na kampuni ya Consolidated Contractors Group kwa gharama ya Dola 82.521 milioni; Kipande cha pili chenye urefu wa kilometa 64.2 kilikuwa kutoka Ikana hadi Laela na kilijengwa na kampuni ya China Newera (64.2km Ikana-Laela) kwa Dola 46.812 milioni; na kipande cha mwisho kilikuwa kutoka Laela hadi Sumbawanga chenye urefu wa kilometa 95.31 ambacho kilijengwa na kampuni ya Aarsleff-Interbeton J.V kwa gharama ya Dola 130.038 milioni. Kwa hiyo kilometa zote 222.71 ziligharimu jumla ya Dola 259.371 milioni ambazo ni fedha za wahisani na fedha za ndani.
Ni fedha nyingi sana lakini haziwezikuzidi thamani halisiya barabara hii ambayo licha ya kuwakomboa wananchi wa pembezoni hasa katika mikoa ya Mbeya, Rukwa na Katavi, lakini pia itasaidia kuiunganisha Tanzania na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sababu ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 112 kutoka Sumbawanga-Matai hadi bandari ya Kasanga katika Ziwa Tanganyika unaendelea chini ya kampuni ya China Railway 15th Bureau Group Corporation – CR15G kwa gharama ya Dola 80.912 milioni.
Dk. Magufuli, ambaye sasa ni mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), anazifahamu karibu barabara zote nchini na hatua zilikofikia. Alipoingia kwa mara ya kwanza bungeni mwaka 1995 baada ya kushinda katika jimbo la Chato akiwa na miaka 36 tu,  Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.
Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk. Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu, wadhifa aliodumua nao hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipomalizika.
Mwaka 2005 alishinda ubunge kwa mara ya tatu, lakini safari hii aliingia katika orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Rais Jakaya Kikwete akamteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 akagombea tena ubunge, lakini safarihii akapambana na mgombea wa Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alitoa upinzani mkubwa ingawa hatimaye Magufuli alishinda kwa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mpinzani wake. Rais Kikwete akamrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.
Tangu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, wengi walikuwa wakimtaja Magufuli kwamba anafaa kuwania urais, lakini yeye alikaririwa akisema wakati huo kwamba hana mpango huo.
Hata makada wenzake walipoanza kuonyesha nia kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu, yeye hakuwa na papara na iliwashangaza wengi Mei 29 alipoamua kujitosa kimya kimya, akachukua fomu na kuondoka, bila mbwembwe wala madoido kama walivyofanya wengine.
Wanaomfahamu wanasema nguvu yake kubwa iko kwenye elimu yake, lakini kukaa muda mrefu kwenye wizara zake na mambo makubwa aliyoyafanya katika wizara alizopata kuziongoza, pamoja na uwezo wake wa kutoa maamuzi magumu kila mara vinampa sifa ya kuwa rais anayefaa katika kipindi hiki ambacho rushwa, ufisadi na ukosefu wa maadili vimetamalaki.
Udhaifu wake pekee unaotajwa na walio karibu yake ni kufanya maamuzi ya haraka, jambo ambalo linaweza kurekebishwa kwa kuwa ndani ya Taasisi ya Urais kuna washauri makini.
UJENZI WA BARABARA
Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya nne, barabara zenye urefu wa jumla ya 6,276.82km zimejengwa kwa gharama ya Dola 102,654.98 milioni, nyingi kati ya hizo zikiwa za lami na hivyo kuutengeneza mtandao imara wa miundombinu ya barabara.
Kujengwa kwa barabara hizo kumerahisisha hata usafiri ambapo leo hii magari ya abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Musoma, Mwanza, Kagera na Kigoma hayahitaji kuzunguka Nairobi bali yanakwenda moja kwa moja.
Hivi sasa usafiri wa kutoka Dar es Salaam kwenda Sumbawanga ni wa siku moja badala ya siku mbili, kama ilivyo kwa usafiri wa Dar es Salaam kwenda Mbinga, jambo ambalo miaka 10 iliyopita lilikuwa ndoto.
Asilimia 90 ya miradi hiyo imesimamiwa na Dk. Magufuli akiwa Waziri wa Miundombinu katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015na bado miradi mingine inaendelea kujengwa japo imesimama kidogo kutokana na ufinyu wa bajeti.
Kampuni za Kichina zimepata mikataba mingi ya ujenzi. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kampuni 14 kutoka China zimeingia jumla ya mikataba 58 ya ujenzi wa kilometa 3,140.85 yenye thamani ya Dola 1.75 bilioni.
Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co., Ltd. (CHICO) ambayo ilipata mkataba wenye thamani ya Dola 206 milioni kutoka Wakala wa Barabara Zambia kujenga barabara ya Mansa-Luwingu yenye urefu wa kilometa 175, peke yake imeingia mikataba 13 nchini Tanzania ya barabara zenye urefu wa kilometa 705.2 zikiwa na thamani ya Dola 490.26 milioni.
Hizi ni pamoja na barabara za Singida-Iguguno (76km) yenye thamani ya Dola 20.55 milioni; Sekenke-Shelui (33km) yenye thamani ya Dola 12.51 milioni; Mwandiga-Manyovu (60km) wenye thamani ya Dola 32.54 milioni; Kigoma-Kidahwe (35.7km) kwa Dola 19.56 milioni; Bonga-Babati (19.20km) kwa Dola 11.95 milioni; Tabora-Urambo (42km) kwa Dola 31.17 milioni; Kyaka-Bugene (59.1km) kwa Dola 51.6 milioni; Dareda-Minjingu (84.6km) kwa Dola 51.6 milioni); Kidahwe-Uvinza-Ilunde (76.6km) kwa Dola 47.5 milioni; Isaka-Ushirombo (132km) kwa Dola 88.223 milioni; Kilwa Road Phase III (1.5km) kwa Dola 3.4 milioni; Nyanguse-Musoma (85.5km) kwa Dola 3.3 milioni; na Kagoma-Lusahunga (154km ) kwa ubia na kampuni ya CRSG kwa gharama ya Dola 116.2 milioni.
China Sichuan International Cooperation Co., Ltd (SIETCO) inajenga barabara zenye urefu wa 283.9km zenye thamani ya Dola 123.03 milioni ambazo ni Isuna-Singida (63km) kwa Dola 18.5 milioni; Tarakea-Rongai-Kamwanga (32km) kwa Dola 8.8 milioni; Iringa-Migori (95.1km) kwa Dola 51.123 milioni; na Migori-Fufu Escarpment (93.8km) kwa Dola 44.7 milioni, wakati kampuni ya CICO inajenga barabara ya Nangurukuru-Mbwemkuru yenye 95km kwa thamani ya Dola 23.82 milioni.
Kampuni ya China Geo-Engineering Corporation International Ltd (CGC INT’L) inajenga barabara zenye urefu wa 525.9km zikiwa na thamani ya Dola 151.2 milioni. Barabara hizo ni Shelui-Nzega (112km) kwa Dola 12.6 milioni; Kyamorwa-Buzirayombo (120km) kwa Dola 29.822 milioni; Manyoni-Isuna (54km) kwa Dola 18.4 milioni; Arusha-Namanga (104.2km) kwa Dola 49.64 milioni; Chalinze-Tanga Phase I (125km ) kwa Dola 25.9 milioni na ndiyo kampuni iliyojenga Daraja la Mkapa (Daraja la Umoja 10.7km) linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa gharama ya Dola 14.9 milioni.
Katika orodha hiyo, ipo kampuni inayomilikiwa na serikali ya China, Hydropower Engineering and Construction Company (SINOHYDRO) ambayo ilipata mikataba 12 nchini Tanzania ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa jumla ya 779.95km zenye thamani ya Dola 434.36 milioni. Barabara hizo ni Sengerema-Usagara (40km) kwa gharama ya Dola 21.724 milioni; Buzirayombo-Geita (100km) kwa Dola 25 milioni; Geita-Sengerema (50km) kwa Dola 24.034 milioni; Dodoma-Mayamaya (43.65km) kwa Dola 25 milioni; Manyoni-Itigi-Chaya (89.3km) kwa Dola 66.56 milioni; Puge-Tabora (56.1km) kwa Dola 35.085 milioni; Handeni-Mkata (54km) kwa Dola 34.81 milioni; Korogwe-Handeni (65km) kwa Dola 38.4 milioni; Katesh-Dareda (73.8km) kwa Dola 38.94 milioni; Singida-Katesh (65.1km) kwa Dola 31.34 milioni; Tanga-Horohoro (65km) kwa Dola 42.43 milioni; na Peramiho Junction-Mbinga (78km) kwa Dola 48.444 milioni.
CHIKO ilijenga barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam yenye urefu wa 4km kwa thamani ya Dola 7.9 milioni, China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ilipata mikataba minne ya kujenga barabara zenye urefu wa 145.6km kwa thamani ya Dola 95 milioni. Barabara hizo ni Magole-Turiani (48.6km) kwa Dola 25.43 milioni; Tabora-Urambo (52km) kwa Dola 36.3 milioni; Dumila-Rudewa (45km) kwa Dola 25.5 milioni na Jangwani Depot kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (BRT) kwa Dola 7.81 milioni.
(Imeandaliwa na www.brotherdanny.com. Simu:0656-331974

Comments