RC ARUSHA AVIOMBA VYOMBO VYA HABARI KUSAIDIA UCHAGUZI MKUU KUWA WA AMANI


Na Woinde Shizza,Arusha
 Mkuu wa mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, amevitaka vyombo vya habari nchini kusaidia uchaguzi mkuu mwaka huu umalizike kwa amani na utulivu ili Tanzania iendelee kuwa na sifa ya amani Barani Afrika.

Akizungumza katika tamasha la 10 la vyombo vya habari mkoani hapa, lililowashirikisha wanahabari kutoka mkoa wa Arusha, Manyara na jijini Dar es Salaam, Ntibenda, alisema vyombo vya habari ni wadau wakubwa wa amani na utulivu.

Alisema kama wanahabari wote watafanyakazi kwa weledi, wanaweza kusaidia Taifa kupita salama katika uchaguzi Mkuu wa mwezi Octoba mwaka huu.
Ntibenda alisema kwa mkoa wa Arusha, suala la amani ni la kipekee hivyo ni muhimu kila mdau kuhakikisha amani inakuwepo, kwani Arusha ndio kitovu cha utalii nchini.Alisema anaunga mkono kauli mbiu za Tamasha hilo, kuwa Uchaguzi mkuu bila vurugu inawezekana.

Hata hivyo, alisema kama wa wanahabari wakifanya kazi kwa ushabiki wa vyama bila kujali maadili wanaweza kuchangia kulitumbukiza taifa katika vurugu.

Awali Mkuu wa Idara ya Matukio ya kampuni ya Bia nchini(TBL), Chris Sarakana aliwataka wanahabari kutumia vyema kalamu zao kuhamasisha amani na utulivu nchini.Naye mmoja wa waandaaji wa Tamasha hilo, Mussa Juma alisema waliamua kauli mbiu katika tamasha hilo la 10, kuwa ni uchaguzi bila vurugu inawezekana, ili kuweza kuhamasisha amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu.


Katika kuhamaisha amani na kukuza utalii wa ndani, wanahabari kutoka Jijini Dar es Salaam walipata fursa kutembelea hifadhi ya Taifa ya Arusha na wanahabari wa mkoa wa Arusha, walitembelea kiwanda cha bia nchini TBL

Comments