EU KUTUMA WAANGALIZI 128 KWAAJILI YA UCHAGUZI MKUU UTAKAOFANYIKA OKTOBA MWAKA HUU

Katibu Mkuu  wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania, Mhe. Filiberto Sebregondi, wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa leo, 28-08-2015, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo.
 Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Filiberto Sebregondi, akisaini Hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, naye akisaini Hati hiyo.
Zoezi la kusaini likiendelea.
Katibu Mkuu,Balozi Mulamula akisisitiza jambo, huku Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, wakifuatilia kwa makini mazungumzo hayo.
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga,(kulia) akizungumza katika hafla hiyo ya kusaini hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Bi. Mindi Kasiga akiwatambulisha waandishi wa Habari, waliohudhuria hafla hiyo (hawapo pichani).
 Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Filiberto Sebregondi, akijibu maswali ya Waandishi wa habari. 
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari.
Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe.Filiberto Sebregondi, akiagana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, muda mfupi mara baada ya kusaini hati hiyo.

NA REUBEN MCHOME.
Umoja wa Ulaya (EU) utatuma timu ya waangalizi yenye wajumbe 128 nchi nzima katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba 2015. 

Hayo yalibainishwa wakati wa uwekaji saini wa Makubaliano ya awali ya kuruhusu timu hiyo kati ya EU na Serikali ya Tanzania uliofanyika kwenye Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tarehe 28 Agosti 2015. 

Uwekaji saini huo umefanywa na Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kwa upande wa EU ulifanywa na Mhe. Filiberto Ceriani Sebregondi, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania.


Akizungumza baada ya uwekaji saini wa Makubaliano hayo,  Balozi Sebregondi alieleza kuwa EU imekuwa ikituma timu hiyo kwa nchi washirika ambazo zina historia nzuri ya demokrasia. Aidha, nchi hizo zina dhamira ya dhati ya kukuza mahusiano na EU kwa kuruhusu waangalizi wafanye majukumu yao katika hatua zote za uchaguzi kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa haki na huru.



Balozi Sebregondi aliendelea kueleza kuwa timu kama hiyo ambayo wajumbe wake wanakuwa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya, ilitumwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo iliutangaza kuwa ni huru na haki.   Timu pia ilitoa ushauri na maelekezo ya namna ya kufanya maboresho katika hatua mbalimbali za uchaguzi.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula aliikaribisha timu hiyo kuja Tanzania na alisema kuwa  jukumu la Wizara yake ni kuratibu na kuhakikisha kuwa wajumbe wa timu hiyo wanatekeleza majukumu yao kama ilivyokubalika kwenye Makubaliano ya Kimataifa. Aliongeza kuwa maelezo ya undani wa shughuli ya timu hiyo wakati wa uchaguzi yatatolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambao pia watasaini makubaliano ya utekelezaji wa kazi ya timu hiyo. 

Taasisi zingine za Kimataifa zinazotarajiwa kutuma timu za uangalizi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).

Comments