Friday, December 11, 2015

NAPE MGENI RASMI TUZO SIKU YA MSANII

.Twanga, K-Mondo Muzika, Mafumu Bilal kutoa burudani
WAZIRI wa Habari, Wasanii, Utamaduni, Vijana na Michezo, Nape Nnauye leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tuzo za Siku Ya Msanii zitakazofanyika kwenye ukumbi wa Makumbusho, Posta, Dar es Salaam.

Hii ni mara ya pili kwa tuzo za Siku Ya Msanii kufanyika, ambapo mara ya kwanza zilifanyika mwaka jana kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.Mwaka huu zitatolewa tuzo nne ikiwa ni nyongeza ya tuzo mbili tofauti za zile za mwaka jana. Mwaka huu zitatolewa tuzo kutoka katika sekta ya filamu, muziki, sanaa za maonyesho na sanaa za ufundi.

Meneja Uhusiano wa Siku Ya Msanii, Petter Mwendapole amesema walipeleka maombi wizarani kuomba Waziri atakayekuwa na dhamana ya Sanaa awe mgeni kwenye tukio la leo.“Kwa hiyo kimsingi baada ya kuapishwa jioni Waziri Nnauye atakuwa kwenye hafla hii na wasanii nao watampa mahitaji yao nay eye akitoa mtazamo wa wizara kuhusu Sanaa nay eye pengine kuyatolea majibu.

 Mwendapole alisema katika burudani kutakuwa Mwanamuziki maarufu Richard Mangustino akiwa na bendi yake ya K-Mondo Muzika, kikundi cha Sanaa cha Safi, Mpuliza Saxaphone  Mafumu Bilal ‘Bombenga’ lakini pia wacheza sarakasi na yoga.Awali bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ watakuwa wanatoa burudani kwenye maonyesho ambao wao watakuwa kwenye burudani za awali sambamba na bendi ya Ifakara Sound kutoka, Ifaraka Morogoro.

Mwaka huu Tuzo hizo, zilianza na maonyesho ya kazi za wasanii ambapo wasanii kutoka mashirikisho manne ya sanaa walionyesha kazi zao katika viwanja vya makumbusho, Dar es Salaam.Mwaka jana washindi wa tuzo za Siku Ya Msanii walikuwa Father Canute Mzuwanda aliyeshinda tuzo ya Humanitarian wakati Said Tingatinga alishinda tuzo ya Life Time Achievement.

Siku Ya Msanii inaandaliwa na Haak Neel Production kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kudhaminiwa na New Habari (2006) LTD kupitia magazeti ya Bingwa, Dimba, Mtanzania na The African. Wadhamini wengine ni Channel Ten, Magic FM na CXC, Kilimanjaro Twist.
Post a Comment