Monday, December 07, 2015

BENKI YA EXIM YAENDESHA DROO YA MWISHO YA KAMPENI YAKE YA AKAUNTI YA MALENGO.

Mmoja wa wateja wa Benki ya Exim Tanzania, Bw Kakili Juma (wa pili kushoto) akiokota karatasi yenye jina la mshindi wa droo ya mwisho na kubwa ya kampeni ya akaunti ya malengo ya Benki ya Exim Tanzania iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni kwa wiki.Wanaoshuhudia kushoto ni pamoja na Meneja Bidhaa ya benki hiyo, Bw Aloyse Maro, Mwakilishi kutoka Bodi ya Taifa michezo ya kubahatisha nchini (GBT), Bw Bakari Maggid, Meneja Masoko wa benki hiyo Bw. Abdulrahman Nkondo pamoja na Ofisa wa benki hiyo Bw. George Musetti.

BENKI ya Exim Tanzania imeendesha droo yake ya mwisho na kubwa ya kampeni ya akaunti ya malengo huku mteja wa benki hiyo Bw.Dileshkumar Solanki mkazi wa wa jijini Dar es Salaam akiibuka mshindi na hivyo kujishindia gari ndogo aina ya Toyota IST. 

Kampeni hiyo ilizinduliwa mwezi Mei mwaka huu ambapo kupitia kampeni hiyo benki hiyo imekua ikitoa zawadi mbalimbali za kila mwezi zikiwemo simu aina ya iPhone 6 kwa wateja waliobahatika kuibuka washindi kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini. 

Akizungumza kwenye hafla fupi ya uendeshaji wa droo hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, Meneja Bidhaa wa benki hiyo Bw Aloyse Maro alisema benki hiyo imeridhishwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wateja wake wakati wote wa kampeni hiyo inayolenga kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba miongoni mwa watanzania. 

“Kampeni hii imekuwa ni yenye mafanikio. Imepokelewa kwa mwamko mkubwa kutoka kwa wateja wetu hatua ambayo tumeitafsiri kwamba ni wazi wateja wetu wananufaika na wanafurahia huduma zetu,’’ alisema Bw Maro muda mfupi baada ya kufanyika kwa droo hiyo iliyosimamiwa na Bodi ya taifa michezo ya kubahatisha nchini (GBT) 

Bw. Maro aliongeza kuwa sambamba na zawadi hizo kampeni hiyo inaambatana na utoaji wa riba nzuri zaidi kwa wateja wanaofungua akaunti hiyo ya malengo. 

“Hatujaishia tu kwenye kutoa zawadi hizi kwenye kampeni hii bali tulihusisha pia utoaji wa riba nzuri zaidi kwa wateja wanaofungua akaunti yetu ya malengo,’’ alibainisha. 
Post a Comment