Thursday, July 30, 2015

TANZANIA YAFANYA KUFURU MBIO ZA NYIKA SARPCCO

SW1
Wanariadha wa mbio za nyika  katika michezo ya majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika(SARPCCO) wakiendelea na mbio hizo jana katika mji wa Mbabane Swaziland ambapo wanariadha wa Polisi Tanzania walifanikiwa kushika nafasi tatu za mwanzo.(Picha na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi-Swaziland)
SW2
Wanariadha wa mbio za nyika  kutoka Polisi Tanzania wakipongezana baada ya kumaliza kukimbia mbio  hizo jana katika mji wa Mbabane Swaziland ambapo michezo ya majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika(SARPCCO) inaendelea. Tanzania walifanikiwa kushika nafasi tatu za mwanzo katika mbio hizo.(Picha na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi-Swaziland)
………………………………………………………………………….
Na. Frank Geofray-Jeshi la Polisi,Swaziland.
Wanariadha wa Polisi Tanzania walioshiriki katika mbio za nyika katika michezo ya majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini (SARPCCO) wamefanya kufuru kwa kuzoa medali zote baada ya kushika nafasi tatu za juu.
Wanariadha waliofanya vizuri na nafasi zao katika mabano  ni pamoja na Basili John (1), Fabian Nelson(2) na      Josephat Joshua(3) ambapo mshindi wa kwanza aliweza kutumia muda wa dakika 29:26:00.
Wanariadha wengine kutoka Tanzania walioshiriki mbio hizo ni pamoja na Osward Revelian, Wilbado Peter, Silvester Naal na Fabiola Willium kwa upande wa wanawake na hivyo kusababisha ushindi wa jumla kwa kupata medali ya dhahabu.
Kwa matokeo hayo timu ya Tanzania inayoshiriki michezo hiyo imefanikiwa kufikisha medali sita za dhahabu, nne za fedha na mbili za shaba na hivyo kujihakikishia nafasi nzuri katika ushindi wa jumla wakati  michezo hiyo itakapofikia ukingoni Agosti pili mwaka huu.
Akizungumzia matokeo hayo Kocha wa Wanariadha hao Rogart Steven alisema wanariadha hao walijiandaa vyema na kujituma licha ya kukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanariadha wa Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini.
 Katika Michezo ya Mwaka huu Tanzania inawakilishwa na Wanariadha kumi na mbili pekee ambao wameonyesha kiwango kikubwa katika mchezo huo ukilinganisha na mataifa mengine ambayo yameleta idadi kubwa ya wanamichezo..

No comments: