Monday, July 27, 2015

UKAWA WAMKARIBISHA EDWARD LOWASSA

unnamed (6) 
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba wakijadilia jambo katika mkutano na waandishi wa habari.
……………………………………………………………………
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umethibitisha tetesi zilizokuwa zikijadiliwa kwenye mitandao ya kijamii nchini juu ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kujiunga na umoja huo ili kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Tamko lililosainiwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kwa niaba ya wenyeviti wenza wa umoja huo wameamua kumkaribisha Lowassa ili aungane nao kwakuwa ni mchapa kazi
Amesema Watanzania wanataka mabadiliko yatakayoibua demokrasia ya kweli kuachana na uonevu, udhalilishaji,  na majungu unaoendelezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Tunaamini Lowassa ana uwezo wa kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki,  mfuatiliaji wa karibu wa utendaji katika majukumu anayokabidhiwa,”  Mbatia ameongeza katika ofisi za Chama cha Wananchi (CUF)  akiwa na wenyeviti wenza Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Emmanuel makaidi (NLD).
“Katika kutafakari kwa kina maslahi ya taifa letu, Ukawa tunahitaji viongozi wenye sifa, uwezo na weledi katika kulinda, kuheshimu na kusimamia rasilimali za taifa kwa maslahi ya Watanzania wote,” alisema Mbatia.
Baada ya kutoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari Mbatia aliulizwa ikiwa wanakumbuka namna viongozi wa vyama vya upinzani walivyomnyooshea kidole Lowassa kutokana na kashfa ya ufisadi Richmond iliyomfanya kujiuzulu wadhifa wake mwaka 2008.
Mbali ya Richmond, Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbroad Slaa akiwa katika uwanja wa Mwembeyanga Temeke jijini Dar es Salaam alitaja orodha ya majina 11 ya mafisadi  jina la Lowassa likiwemo je ikiwa kiongozi huyo atajiunga na Ukawa watawaambia nini Watanzania kuhusiana na usafi wake.
Mbatia alisema, “Ufisadi ni masuala ya kimfumo, mfumo uliopo CCM ndio unaolea ufisadi.
Emmanuel Makaidi alisema Ukawa hawawezi kuthibitisha kama Lowassa ni fisadi au la mpaka vyombo vya sheria vitakapomtangaza.
“Kuna watu wengi wapo gerezani na wengine kesi zinaendelea mahakamani kutokana na ufisadi, lakini hatujaona kesi ya Lowassa utasemaje ni fisadi,” alisema Makaidi.
Kuhusu nafasi ya Lowassa kugombea urais kupitia Ukawa Profesa Lipumba alisema kwa sasa hawajampitisha moja kwa moja, lakini atakapokubali kujiunga watakaa na kujadiliana kwa mujibu wa katiba yao halafu watajua kama awe mgombea wao au vinginevyo.

No comments: