OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YAENDESHA MAFUNZO YA UTAFITI WA AFYA YA UZAZI NA MTOTO NA MALARIA TANZANIA MKOANI KILIMANJARO

TA1
Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii akiwahutubia washiriki wa mafunzo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.
TA2
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akitoa maelezo ya awali wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.
TA3
Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii akizindua matokeo muhimu ya Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma ya Afya Nchini wa mwaka 2014/2015 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.
TA5
Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii akimkabidhi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Andrewleon Quaker kijitabu cha matokeo muhimu ya Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma ya Afya Nchini wa mwaka 2014/2015 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika  Moshi, mkoani Kilimanjaro.
……………………………………………………………………………..
Na: Veronica Kazimoto, MOSHI
Afya ya Uzazi na Mtoto ni viashiria vizuri vinavyoonyesha maendeleo ya uchumi na kijamii na vinaainishwa na utoaji endelevu wa huduma za afya nchini.
 
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii wakati akifungua rasmi mafunzo ya Wasimamizi, Wahariri na Wadadisi wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.
 
“Kutokana na umuhimu wa viashiria hivyo, Serikali kupitia Mpango wake wa Afya ya Uzazi na Mtoto imefanya juhudi za ziada katika kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na matatizo ya uzazi na vifo vya watoto wachanga nchini”, Amesema Dkt. Rusibamayila.
 
Dkt. Rusibamayila amesema kuwa vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vimeendelea kupungua ambapo kwa mwaka 2012 kulikuwa na vifo 432 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa hai ikilinganishwa na vifo 454 kwa kila watoto waliozaliwa hai 100,000 iliyopatikana kwenye Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa mwaka 2010.
 
Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 51 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai kama ilivyopatikana kutoka kwenye Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa mwaka 2010 na kufikia vifo 45 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai kwa mwaka 2012.
 
Aidha, Dkt. Rusibamayila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo amewaasa washiriki hao kufanya kazi yao kwa weledi ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata takwimu sahihi za  Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 kwa ajili ya kupanga maendeleo.
 
Pamoja na ufunguzi wa mafunzo hayo, Mgeni rasmi huyo amezindua matokeo muhimu ya Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma ya Afya Nchini wa mwaka 2014/2015.
 
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa, vituo saba (07) kati ya kumi (10) vinatoa huduma zote za msingi za afya yaani tiba kwa watoto, chanjo pamoja na ufuatiliaji wa mwenendo wa ukuaji wa mtoto.
 
Aidha, huduma za matibabu kwa watoto wagonjwa zinapatikana kwa asilimia 98   katika vituo vyote vinavyotoa huduma za afya Nchini, pia zaidi ya vituo vinane (8) kati ya kumi (10) nchini vinatoa huduma za chanjo kwa watoto.
 
Kwa huduma za kisasa za uzazi wa mpango zinapatikana kwa asilimia 80 ya vituo vyote vinavyotoa huduma za afya, ikilinganishwa na asilimia 76 kwa utafiti wa namna hii wa mwaka 2006.
 
Aidha,  kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2014/2015 karibu vituo vyote vya Serikali (sawa na asilimia 97) vinatoa huduma za uzazi wa mpango ikilinganishwa na asilimia 35 ya vituo binafsi vya kibiashara na asilimia 41 ya vituo vinavyomilikiwa na asasi za kidini.
 
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo amesema utafiti huu wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015  unalenga kukusanya taarifa nyingi za sekta ya afya zinazotumika katika kutathmini malengo mbalimbali na pia kusaidia katika kupanga mikakati mipya.
 
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mara nyingine tena inafanya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 ambao kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2010. Utafiti huu utaanza rasmi mwishoni mwa mwezi Agosti, 2015 kwa nchi nzima yaani Tanzania Bara na Visiwani.

Comments