Katibu wa Taasisi ya Zanzibar Heart Foundation Sururu Abass Othman akizungumza na wananchi wa shehia za Muembemakumbi, Karakana na Chimbuni waliofika kuchungaza Afya zao.
Picha na Makame Mshenga Maelezo Zanzibar
Mratibu wa Muungano wa Taasisi zinazoshughulikia maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (ZNCDA) Omar Abdalla Ali akiwaelimisha wananchi waliofika kituo cha Afya Karakana kuchunguza afya juu ya maradha ya maradhi hayo na njia bora za kujikinga.
Muuguzi wa Kituo cha Afya Karakana Mere Hamad Jadi akiwapima wananchi maradhi ya sindikizo la damu wakati wa zoezi hilo lililofanyika Kituo cha Afya cha Karakana nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
…………………………………………………………….
Na RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR.
Muungano wa Taasisi zinazoshughulikia maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (ZNCDA) umeishauri Serikali na Mashirika wahisani kuelekeza nguvu zao katika mapambano dhidi ya maradhi hayo kwa vile hivi sasa yamekuwa tishio kwa maisha ya wananchi kuliko maradhi mengine yoyote Zanzibar.
Mratibu wa ZNCDA Omar Abdalla Ali alitoa ushauri huo wakati wa zoezi la kuwapima afya wananchi wa shehia za Karakana, Chimbuni na Muembemakumbi, Mkoa Mjini Magharibi Unguja, lililofanyika Kituo cha Afya cha Karakana.
Alisema maradhi ya Sindikizo la damu, Kisukari na Saratani yamejitokeza kuwa tishio kwa wananchi kutokana na uelewa wao mdogo juu ya maradhi hayo na wengi kutokuwa na mwamko wa kupima afya zao.
Alizitaja sababu zinazochangia kuongezeka maradhi yasiyoambukiza kuwa ni mabadiliko ya mfumo wa maisha ambao wananchi hupenda zaidi starehe kuliko kujituma, uvutaji sigara, ulevi wa kupindukia na kutumia chakula cha makopo kilichotiwa kemikali.
Akitowa takwimu ya maradhi hayo, Omar alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2011 asilimia 33 ya wananchi wa Zanzibar wanakabili na sindikizo la damu na asilimia nne wanamaradhi ya kisukari na taarifa kutoka Hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam zinasema kuwa kila mwaka wanapokea kiasi cha wagonjwa 1000 wa magonjwa ya saratani kutoka Zanzibar.
Aliongeza kuwa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa akinamama na tenzi dume kwa wanaume zinaongoza kati ya wagonjwa wanaopelekwa huko kupatiwa matibabu.
Alisema taarifa hizo zinatisha kutokana na idadi ndogo ya wananchi wa Zanzibar na ni sababu iliyopelekea ZNCDA kufanya juhudi ya kutoa taaluma kwa wananchi, kuwapima afya ndani ya shehia zao na kuwapa ushauri unaofaa wa kujikinga na maradhi hayo.
Aliwataka wananchi kuanzisha utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kujua afya zao mapema badala ya kusubiri kuathiriwa na maradhi ndipo wakimbilie Hospitali.
“Maradhi yanapogundulika mapema ni rahisi kuyatibu lakini unaposubiri mpaka yakakuathiri inakuwa vigumu kuyatibu pimeni afya zenu kila wakati, ” alisisitiza Mratibu wa ZNCDA.
Aliwashauri viongozi wa Serikali za mitaa, wabunge ,wawakilishi na madiwani, kuwasaidia wananchi kwa kuwawekea vifaa vya kupima afya zao katika sehemu wanamoishi kwa vile vifaa hivyo havina gharama kubwa.
Jumla ya wananchi 174 kutoka shehia hizo tatu walipata nafasi ya kuangaliwa afya zao na maradhi ya sindikizo la damu yamegundulika kuongoza katika shehia hizo.
Comments