JAIRO, KILLIMBAH,GYUNDA WAGOMEA MCHAKATO KURA ZA MAONI UBUNGE IRAMBA, WAMTAKA KATIBU CCM WILAYA KUACHA KUMBEBA KWA MBELEKO MWIGULU NCHEMBA

2
Mmoja wa wagombea wa Ubunge Jimbo la Iramba, Mkoani Singida Davd Jairo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani, juu ya madai yao ya kugomea kuendelea na mchakato wa kura za maoni hadi msimamizi wa uchaguzi ambae ni katibu wa CCM Wilaya ya Iramba Mathias Shidagisha aondolewe kwenye zoezi hilo, kulia ni David Jairo na kushoto ni Amon Gyunda .
3
Mmoja wa wagombea wa Ubunge Jimbo la Iramba, Mkoani Singida Juma Killimbah akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye ofisi za chama cha waandishi  wa habari Mkoani humo Singpress.
4
Kilimbah akionesha waandishi mojawapo ya sms za M pesa zlizotumwa na Mwigulu kwa Mmoja wa wapiga kura ili kumchagua yeye.
…………………………………………………………..
Na Hillary Shoo, KIOMBOI.
WAKATI  zoezi la wagombea Ubunge kujinadi na kuomba kura kwa wananchi likiendele kote nchini ,hali sio shwari ndani ya CCM  Wilaya ya Iramba, baada ya wagombea watatu kati ya wanne kutangaza kugomea mchakato wa kura za maoni kwa madai kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Iramba anambeba waziwazi  mgombea  mwezao Mwigulu Nchemba.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana na kutoa tamko kwa chama Mkoa wagombea hao, David Jairo, Juma Killimbah na Amon Gyunda  wamesema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na msimamizi wa uchaguzi kura za maoni katika jimbo hilo, ambaye ni Katibu wa CCM Wilaya ya Iramba, Mathias Shidagisha na msaidizi wake, Mwita Raphael, kuwachezea rafu mbaya.
Jumba Killimbah alidai kuwa mgombea mwenzao Mwigulu Nchemba amekuwa akivunja kwa makusudi kanuni na taratibu za mchakato wa uchaguzi huo huku viongozi wa kamati ya Siasa wakifumbua macho hali hiyo.
“Kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Feb 2010, fungu la 3 kanuni ya 17 (v) (1) kimeeleza bayana namna ya kura ya maoni na mikutano mikuu ya kampeni ya matawi itakavyotendeka ambapo inasisitiza wahusika ni wanachama tu.” .Alisema na kuongeza;
“Lakini kwa utaratibu usio rasmi, mikutano hiyo jimboni kwetu ni ya hadhara isiyozingatia akidi ya wanachama na kunakuwepo na wanachama kutoka vyama pinzani ambao hushiriki kikamilifu kuuliza maswali kwa wagombea”.
Aidha, alidai kuwa msimamizi huyo amekuwa akitumia gari la Mwigulu kusambaza mabango yake hadharani kwenye kata mbali mbali huku akitoa maelekezo kwa makatibu wote wa matawi  kuhakikisha Mwigulu anashinda.
 “Pia amekuwa akimruhusu mgombea huyo kuambatana na magari yasiopungua 10, pikipiki 100, baiskeli zisizo na idadi na kuhama na wapambe wake kila eneo la mkutano huku akitumia gari kubwa lenye vipaza sauti” alisema Killimbah.
Aidha alidai kuwa  Shidagisha amekuwa akidiriki kubariki matusi wanayotukanwa na mgombea mwenzao Mwigulu licha ya kulalamika mra kwa mara lakini Katibu huyo amekuwa  akiwataka watwangane wawezavyo mbele ya wapiga kura wao.
Hata hivyo walidai kuwa Mwigulu amekuwa akitumia gari ya umma wa Wizara ya fedha yenye namba za usajili STL 3400 aina ya Land cruiser, gari ambalo alitumia siku ya kuchukua fomu likiwa na namba NW FH.
“Kwa kuwa ni dhahiri msimamizi huyu hawezi kutenda haki na hasa ya kusimamia matokeo ya uchaguzi na kwa kuwa ameshatamka bayana tena kwa viapo na huku akitishia kuwapiga baadhi ya  wagombea , sisi kama wagombea tumeonelea tumkatae ndugu Shidagisha na msaidizi wake Mwita Rafael kuendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi Jiimbo la Iramba, sambamba na kuchukuliwa hatua za akimaadili na pia Katibu wa UVCCM Wilaya Abel Makala kuacha kuwa kampeni meneja wa Mwigulu huku akitumia wadhifa wake.” Alifafanunua Jairo.
Hata hivyo Killimbah alionesha waandishi wa habari sms inayoonesha kuwa Mwigulu alimtumia mmoja wa wajumbe fedha kiasi cha shilingi laki moja kama njia mojawapo ya kumshawishi kumpigia kura.
Akizungumzia malalamiko ya wagombea hao,Kaimu Katibu wa CCM Mkoa  wa Singida Aluu Segamba alisema ni kweli yapo na kwamba  sekretarieti ya mkoa ilitarajiwa kwenda Wilayani Iramba jana kushughulikia suala hilo.
 “Hizi ni changamoto za uchaguzi na hawa ni watu wazima, ni imani yangu tutafikia muafaka maana tutawaita wagombea wote pamoja na kamati ya Siasa ya Wilaya ili tumalize tatizo hili haraka iwezekanavyo.”. Alisema Segamba.

Comments