RAIS KIKWETE AMKABIDHI MLEMAVU BAJAJI MJINI DODOMA



Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi bajaji mpya mlemavu wa miguu ambaye ni mfanyakazi wa TANROADS Bi.Sarah Nalingigwa Nkumbo huko ikulu mjini Dodoma(picha na Freddy Maro) 





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumapili, Februari 10, 2013 amekabidhi pikipiki aina ya bajaj kwa mama mmoja mlemavu, Mama Sarah Mkumbo Nalingigwa katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu Ndogo mjini Dodoma.
Mama Nalingigwa ni mtumishi wa Wakala wa Barabara nchini – TANROADS- katika Mkoa wa Singida na shughuli ya leo imehudhuriwa pia na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mufugale na Mama Salma Kikwete.
Shughuli ya makabidhiano ya leo, inatimiza ahadi ambayo Mheshimiwa Rais aliitoa kwa Mama Nalingigwa wakati alipokutana naye miongoni mwa wananchi waliohudhuria sherehe ya utiaji jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni-Itigi=Chaya mjini Itigi, Mkoa wa Singida Novemba mwaka jana.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi pikipiki hiyo, Rais Kikwete amemwambia mama huyo: “Nimefurahi kwamba nimeweza kutimiza ahadi yangu. Hii ndiyo faraja yangu kwamba sasa utaweza kufanya kazi zako kwa urahisi zaidi, utaweza kutembea kwa urahisi zaidi na kufika kazini na kurejea nyumbani kwa namna ya haraka zaidi.”
Naye Mama Nalingigwa amemwambia Rais Kikwete: “Wewe ni kiongozi shupavu, kiongozi hodari na mpiganaji anayemjali kila mtu. Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akujalia ili uendelee kuwaona wengine wenye mahitaji kama ya kwangu.”
Ameongeza mama huyo ambaye amefanya kazi Wizara ya Ujenzi kwa miaka 30 iliyopita: “Kwa kuniwezesha kiasi hiki, umenipa uwezo wa kufanya kazi kwa namna bora zaidi., Ni vyema kuwa viongozi wengine wakaiga mfano wako wa kujali watu walioko chini yako.”
Amesisitiza: “ Sisi walemavu tuna mahitaji mengi na hivyo naomba unedelea kutuangalia kwa jicho la huruma na kutupunguzia vikwazo vya maisha kila nafasi inapojitokeza.

Comments