Katibu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Thomas Kashilila akitoa somo kwa waandishi wa habari
kuhusu umuhimu wa wabunge kuzisoma na kuzitumia ipasavyo kanuni za bunge
ili kuondoa manug'uniko yanayojitokeza pindi wanapozuiliwa na spika kuchangia
mijadala au kutoa hoja bungeni kwa sababu ya kukiuka kanuni na umuhimu wa
waandishi wa habari kuzitumia taarifa rasmi za bunge katika utoaji wa
taarifa zao.
*********************************************
SIKU chache baada ya Spika wa Bunge, Anne
Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, kulalamikiwa kwa kuendesha Bunge kinyume cha
kanuni, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, amewatetea huku akiwatwisha
lawama hizo baadhi ya wabunge.
Kutokana na kadhia hiyo ya kukosolewa, Dk.
Kashililah alisema kuwa Bunge linaandaa utaratibu wa kusitisha vikao vya Bunge
kurushwa moja kwa moja (live) ili kuzuia purukushani za wabunge kuonekana kwa
wananchi.
Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari katika
Ofisi za Bunge jana kuhusu shughuli zilizotekelezwa katika Mkutano wa Kumi wa
Bunge na mapendekezo ya kuundwa kwa kamati mpya, Dk. Kashililah alisema vurugu
zilizojitokeza zilitokana na kutofuatwa kwa kanuni ambazo zipo wazi.
Alisema vurugu zinazotokea ni kutokana na baadhi
ya wabunge kutozifahamu vema kanuni au kufanya makusudi, hasa kanuni ya 60 na
68, ambazo kama zingefuatwa hayo yote yasingetokea.
Dk. Kashililah alisema baadhi ya wabunge
walikuwa wakishindwa kufuata kanuni kwa makusudi kwa kutumia kifungu kimoja tu
cha 68 cha kuomba taarifa, utaratibu au mwongozo bila ya kufuata taratibu
zinavyotakiwa badala ya kuombea kanuni iliyovunjwa kwanza ndipo aseme yake.
“Mfano, mbunge anajua kuwa anatakiwa kutumia
kanuni ya 68 kuomba taarifa, utaratibu au mwongozo, atasimama, baada ya
kusimama ataambiwa na Spika aseme, naye atasema amesimama kwa kanuni ipi na
anachoombea taarifa ni nini. Lakini baadhi yao wakiomba tu utaona kabla ya
kuruhusiwa hapohapo wanaanza kuzungumza,” alisema.
Aliongeza kuwa hali hiyo ya kuzijua kanuni na
kutozifuata ndiyo inasababisha kuwapo kwa vurugu hizo ambazo wakati mwingine
kwa kutumia kanuni hizo hizo zinamtaka Spika ama aliyekalia kiti chake
kuahirisha Bunge.
Dk. Kashililah alisema wanaamua kutoonesha vikao
vya Bunge moja kwa moja kutokana na baadhi ya wabunge kukiuka kanuni, kwa
kuzungumza mambo yasiyofaa ili waonwe na wapiga kura wao.
“Bunge ni sehemu ya siasa, na mule ndani zimo
pande mbili zinazovutana na kwa wale wabunge waopenda kamera ya televisheni
utawaona wanazungumza mambo yasiyofaa hadi mishipa inawasisima ili waonwe na
wapiga kura wao, mkitoka na kuwauliza watakwambia ni siasa ile.
“Kina mama ambao wanajua kuwa siku hiyo
watauliza maswali utawaona siku hiyo wanavalia kikweli kweli ili waonekane…kwa
kweli sisi tunaokaa tunaona mambo mengi na mengine yanasikitisha,” alisema.
Alisema walipoomba kuzima, baadhi yao walitoa
onyo kwamba waache, ila Bunge linajipanga kufanya utaratibu wa kukaa na Mamlaka
ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuliwezesha Shirika la Utangazaji la Taifa na
televisheni nyingine namna ya kurusha shughuli za Bunge.
“Tunataka kukaa na TCRA, TBC na televisheni
nyingine pamoja na waandishi wa magazeti kuangalia namna ya kuweka maadili ya
kazi, kwa sababu hata TBC wakati mwingine hawafuati maadili, wanampiga picha
Spika Makinda akiwa ameinama huku ikionekana amelala,” alisema. SOURCE:
Tanzania Daima
Comments