Friday, January 08, 2016

WAZIRI PROF. MBARAWA ASISITIZA UWAZI NA UADILIFU TEMESA

2 (2)
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka watendaji na wafanyakazi wote wa Wakala wa ufundi na umeme (TEMESA), kufanya kazi kwa umoja, uwazi na 
uadilifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuhuisha ustawi wa wakala huo.
Akitoa mwelekeo wa utendaji wa wakala huo wakati akizungumza na watendaji wa TEMESA Mhe.Prof. Mbarawa amesema Serikali ya awamu ya tano inaitaka TEMESA kufanya kazi kwa weledi ili kuongeza mapato na kuhudumia wateja wao  kikamilifu ili kuinua uchumi wa wakala huo na kuondoa malalamiko kwa wadau na watumishi.
‘Acheni kufanya kazi kwa upendeleo na usiri kwani huo ndio mwanzo wa hujuma na ubadhirifu hali inayochochea malalamiko na kudumaza huduma za TEMESA’, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameitaka TEMESA kuhakikisha inatengeneza magari ya wadau wote kwa wakati na kutoa huduma za vivuko kwa ufanisi na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kukuza mapato na kuboresha huduma za ufundi na umeme.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sehemu ya ujenzi eng. Joseph Nyamhanga  ameitaka TEMESA kuongeza bidii Katika kukusanya madeni yake ili ipate uwezo wa kibiashara na hivyo kumudu ushindani wa kibiashara.
Naye Mtendaji mkuu wa TEMESA Eng. Marceline Magesa amemhakikishia Waziri  Mbarawa kuwa TEMESA inaendelea na mkakati wa kujenga vivuko vipya viwili ili kuongeza huduma hiyo katika eneo la Magogoni jijini Dar es salaam na Pangani mkoani Tanga.
Aidha amemhakikishia Waziri kuwa ukarabati wa vivuko unazingatiwa na uboreshaji wa karakana unaendelea ili kuvutia wadau wengi kutengeneza magari yao katika karakana hizo.
Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA ulianzishwa mwaka 2006 kwa lengo la kusimamia huduma za ufundi, umeme na usimamizi wa vivuko ambapo hadi sasa takriban vivuko 28 vinasimamiwa na wakala huo nchini kote.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: