Wednesday, January 13, 2016

WAZIRI MKUU AMPA POLE MAMA MARIA NYERERE

LE4
WAZIRI MKUU,Kassim Majaliwa amemtembelea na kuampa pole  mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Maria Nyerere kwa kufiwa na mkwewe  Leticia Nyerere.
Akizungumza na mama Maria alipomtembelea nyumbani kwake jana(Jumanne, Januari 12,2016), Msasani jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu ametoa pole kwa  Mama Maria Nyerere pamoja na familia  na kuwaomba waendelee kuwa  wavumilivu katika kipindi hiki kigumu baada ya 
kuondokewa na mpendwa wao.
“Kipindi hiki ni kigumu, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kila jambo, pia tutajumuika nanyi katika kipindi hichi chote, tuendelee kuwa watulivu na kumwomba Mungu” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Ndugu wa marehemu, John Shibuda (aliyewahi kuwa mbunge wa CHADEMA) ameeleza kutokea kwa msiba huo. Ambapo amesema “Desemba, 19 mwaka huu Leticia Nyerere alipelekwa nchini Marekani kwa matibabu na alifariki dunia katika hospitali ya Doctors Community iliyopo Lanham, Maryland juzi saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Aidha, Shibuda amemshukuru Mheshimiwa Rais John Magufuli kwa kwenda kuipa pole familia na Serikali kwa namna ambavyo inatoa ushirikiano mzuri kwa familia.
 Naye, Rose Nyerere amesema familia inaendelea na maaandalizi, hivyo watatoa taarifa ya baada ya kuandaa utaratibu wa siku ambayo mwili utaletwa nchini, kuagwa na hatimaye kuzikwa Butiama.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ambaye amelazwa siku kadhaa zilizopita katika Taasisi ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu Majaliwa,  amesema amefarijika baada ya kumuona Waziri Mkuu huyo mstaafu akiendelea vizuri na kuwashukuru madaktari na wauguzi kwa kumpatia matibabu na kumhudumia vizuri.  Pamoja na kumpa pole, Waziri Mkuu amemwombea apone haraka ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kila siku.
Naye, Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kumtembelea hospitalini hapo, pia ameipongeza Serikali kwa jitihada mbalimbali inazofanya ili kusaidia wananchi na hatimaye kuiletea nchi maendeleo.
“Naipongeza Serikali kwa namna ambavyo inaendelea kutekeleza majukumu yake katika masuala mbalimbali yenye lengo la kusaidia wananchi” alisema Sumaye.
Waziri Mkuu Majaliwa, pia amemtembelea na kumjulia hali Balozi Hassan kibelloh ambaye amelazwa na anaendelea kupatiwa matibabau katika Taasisi ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

No comments: