Tuesday, January 26, 2016

RAIS MAGUFULI AMPONGEZA RAIS MSTAAFU KIKWETE

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz              

Faksi: 255-22-2113425
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki-moon kuunda jopo la watu mashuhuri watakaomshauri juu ya namna bora ya kuendeleza na kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu hususani katika afya ya uzazi ya Mama na mtoto.

Jopo hilo la watu mashuhuri linaongozwa na wenyeviti wenza ambao ni Rais wa Chile Mheshimiwa Michelle Bachelet na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam Desalegn, huku Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Finland Mheshimiwa Tarja Halonen wakiteuliwa kuwa wenyeviti mbadala.

Katika Pongezi hizo Rais Magufuli amesema kuteuliwa kwa Rais Kikwete kuwa miongoni mwa jopo la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumeijengea heshima Tanzania na kumechochea matumaini ya mafanikio ya kukabiliana na changamoto za afya ya mama na mtoto hususani kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Rais Magufuli ameahidi kuwa serikali yake ya awamu ya tano itatoa ushirikiano katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ambayo jopo hilo litamshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikiwemo katika kuimarisha afya ya uzazi wa mama na mtoto.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

25 Januari, 2016
Post a Comment