Friday, January 15, 2016

DKT. KIJAJI ATOA SIKU 3 KUPATA MIKAKATI YA NAMNA YA KUTATUA SUALA LA UBADILISHANAJI WA FEDHA UNAOFANYWA KIHOLELA (BLACK MARKET) TUNDUMA

va1
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akishauriana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro (kulia) namna ya kutatua changamoto ya usafirishaji mizingo katika forodha ya Tunduma.
va2
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Kijaji (kushoto) akiongea na watendaji wa TRA Mbeya alipowatembelea ofisini kwao kujua matarajio yao pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika utendaji kazi. Kulia kwake ni Bw. Lucas Mnabi Kaimu Meneja TRA Mbeya.
va3
Mkuu wa Hazina Ndogo Mbeya Bw. Siwale (aliyesimama) akitoa ufafanuzi kwa Mhe. Dkt. Kijaji namna wanavyowahudumia wastaafu. Na kushoto kwake ni wafanyakazi wa Hazina Ndogo Mbeya.
va4
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Kijaji (katikati) akiandika dondoo za ujio wake katika ofisi za Mhakikimali Mkoa wa Mbeya. Aliyesimama ni Katibu wa Naibu Waziri Fedha na Mipango na Mchumi Bw. Moses Dulle akitoa utangulizi kabla ya kuanza majadiliano. Kulia ni Mhakikimali Mkoa wa Mbeya Bw. Simon Njoka na pembeni yake ni Mkuu wa Hazina Ndogo Mbeya Bw. Siwale.
……………………………………………………………………………………………
Akizungumza na Meneja wa  Oparesheni ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Benki Kuu Mbeya Bw. Ibrahim Malongo, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alisema kumekuwa na ubadilishanaji fedha isio halali unaofanyika kiholela hapa Tunduma unaopelekea Serikali kukosa mapato.
Mhe. Dkt. Kijaji alifanya ziara hiyo eneo la tukio huko Tunduma na kujionea namna vijana hao wanavyofanya biashara hiyo bila wasiwasi wowote huku wakiwa wameshika fedha nyingi sana mikononi.
“Nakupa siku tatu, nataka unijulishe hali hii (black market) iko vipi kwa sasa, mikakati gani ambayo mmeipanga kwa sasa, nini kimefanyika na hatua gani zimechukuliwa ili kuiwezesha Serikali kupata mapato.” Mhe. Dkt. Kijaji alimwambia na kumsisitiza Meneja wa Oparesheni ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Benki Kuu Mbeya Bw. Ibrahimu Malongo.
Katika ziara hiyo Mhe.  Dkt. Kijaji aliutaka uongozi wa Benki Kuu Mbeya kufuatilia wakopeshaji wanaojiendesha kinyume na taratibu kwa kuwakopesha wananchi tena kwa riba kubwa bila kulipa kodi.
Hivyo amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Bw. Malongo na amempa siku saba kulifuatilia suala hilo kwa karibu, kujua wakopeshaji hao wako wangapi, na wana mikakati gani ya kuiweka kihalali biashara hiyo ili wakopeshaji hao waweze kusimamiwa kwa sheria kanuni na taratibu bila kumuumiza mwananchi na waweze kulipa kodi.
Mhe. Dkt. Kijaji alishauri Taasisi zilizorasmi ambazo zinakopesha kupunguza masharti yasiyo na tija ili kuwasaidia wananchi waweze kukopesheka na waweze kulipa ili maisha yao yaweze kuendelea.
Katika ziara yake Mhe. Dkt. Kijaji alipata fursa ya kuonana na uongozi wa TRA, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro, Hazina Ndogo na alipata fursa ya kuongea na Mkuu wa Hazina Ndogo Bw. Siwale pamoja na Mhakikimali Mkoa wa Mbeya Bw. Simon Njoka. Aliwasisitiza kufanya kazi kwa bidii na kuwataka wawe jicho la Serikali ndani ya Mbeya kwa kuangalia hasa utendaji kazi na kusimamia maadili ya kazi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Fedha

No comments: