Wednesday, January 20, 2016

JAJI LUBUVA AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA NEC

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji Mstaafu Damian Lubuva (kushoto) ambaye ni mgeni rasmi wa mkutano huo, akiongea na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa NEC (hawapo pichani) leo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam kuhusu masuala ya maadili na na ufanisi kazini.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bwana Ramadhani Kailima akiongea na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa NEC (hawapo pichani) leo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam kuhusu masuala ya maadili na na ufanisi kazini kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza 
 
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bwana Ramadhani Kailima wakazi akizungumza katika ukumbi wa mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam leo.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO).


· Awataka kuzingatia maadili na Kanuni za Utawala bora na maadili katika utendaji kazi,
· Awataka kuepukana na rushwa na kushinda vishawishi vya rushwa.

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji Mstaafu Damian Lubuva amewataka Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa NEC kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi ikiwemo kuzingatia maadili na kanuni za Utawala Bora na kuepukana na rushwa.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dar es Salaam wakati alipofungua Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza la Wafanyakazi na kuongea na Wajumbe wa Tume hiyo pamoja na Wajumbe wengine wa TUGHE ngazi ya Taifa na Matawi.

Jaji Lubuva amesema kuwa, Mabaraza ya Wafanyakazi yameundwa Kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi ya Taasisi ili kusimamia rasilimali pamoja na utekelezaji wa majukumu ya Taasisi husika, hivyo kufanyika kwa mkutano huo ni moja ya chachu ya kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi na tija katika Taasisi hiyo.

Akizungumzia kuhusu masuala ya rushwa, Jaji Lubuva ameeleza kuwa, moja ya jukumu la NEC ni kuimarisha na kukuza demokrasia na Utawala Bora, hivyo watumishi wa Tume hiyo hawanabudi kuzingatia maadili na kanuni za utawala bora na maadili katika utendaji wa kazi zao pamoja na kuepukana na vitendo vya rushwa na vishawishi vyake.

‘’Nimeambiwa kuwa, katika kikao hiki mtajadili kuhusu mada mbalimbali kama vile Taratibu za Utendaji kazi Serikalini, masuala ya uanzishaji SACCOS, Utekelezaji wa Bajeti na miradi ya Maendeleo, Ukimwi, Bima ya Afya na masuala ya Madawa ya kulevya, niwaombe kujadili mada hizo kwa kina na busara huku mkitambua kuwa matokeo ya majadiliano yenu ni kwa ajili ya maslahi ya Taasisi yetu na Taifa kwa ujumla’’, alisema Lubuva.

Kwa upande mwingine, Jaji Lubuva amewataka wajumbe wa Baraza hilo kujadili masuala ya afya kwa Wafanyakazi hususani suala la ugonjwa waUkimwi katika sehemu ya kazi ambapo aliwaasa kila mfanyakazi kujikinga dhidi ya janga hilo kwa kulinda afya yake na ya familia yake ili Taifa liweze kunufaika na nguvu kazi iliyopo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Ramadhani Kailima ameitaka jamii kuondokana na dhana potofu dhidi ya Tume hiyo kuwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu na chaguzi ndogo zilizofanyika Tume hiyo imekuwa haina kazi ya kufanya mpaka uchaguzi mwingine kwa kufafanua kuwa, Tume hiyo ina majukumu mengi hata baada ya uchaguzi ikiwemo Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, Uandaaji na Uratibu wa Kura za Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, Uratibu wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi.

‘’Sio kweli kwamba Tume ya Uchaguzi mara bada ya Uchaguzi Mkuu na chaguzi nyingine ndogo zilizofanyika kwamba ndo basi hatuna cha kufanya, Tume ina majukumu mengi hata baada ya uchaguzi kama vile Uratibu na Usimamizi wa Utungwaji wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Uundaji wa Mpango Mkakati wa Tume, Uandaaji wa Rasimu ya Mkataba wa Huduma kwa wateja, Usimamizi wa Ujenzi wa Jengo la Tume na Usimamizi wa chaguzi ndogo pale zinapojitokeza na Mrekebisho ya Muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi’’, alisema Kailima.


Mkutano huo umefunguliwa leo ukiwahusisha Watumishi wa Taasisi toka NEC, Wajumbe wa TUGHE ngazi ya Taifa na Matawi ambao jumla yao ni 54.

No comments: