SERIKALI YAWATAKA WATUMISHI WATAKAOSHIRIKI ZOEZI LA UKUSANYAJI TAARIFA ZA TATHMINI YA KAZI KUWA WAADILILIFU

  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akifungua mafunzo kwa timu ya ukusanyaji taarifa za tathmini ya kazi (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa jengo la Maendeleo ya Jamii Dar es Salaam jana. Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma Bibi Tamika Mwakahesya na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Maendeleo ya Jamii, Bwana James Kibamba.
 Katibu Mtendaji wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma, Bibi Tamika Mwakahesya (kulia) akimkaribisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) kufungua mafunzo kwa timu ya ukusanyaji taarifa za tathmini ya kazi kwenye ukumbi wa jengo la Maendeleo ya Jamii Dar es Salaam jana.
 Timu ya washiriki wa ukusanyaji taarifa za tathmini ya kazi wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mafunzo ya ukusanyaji taarifa za tathmini ya kazi kwenye ukumbi wa jengo la Maendeleo ya Jamii Dar es Salaam jana.
Picha ya pamoja

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi Dkt. Larean Ndumbaro amewataka Watumishi watakaoshiriki zoezi la ukusanyaji taarifa za tathmini ya kazi kufanya kazi hiyo kwa uadililifu mkubwa ili kuweza kupata tathmini sahihi ya mishahara ya watumishi wa umma nchini kulingana na majukumu waliyonayo. 

Katibu Mkuu aliyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya ukusanyaji taarifa za tathmini ya kazi yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Maendeleo ya Jamii jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ndumbaro alisema kuwa kazi ya ukusanyaji taarifa za tathmini ya kazi ni kubwa hivyo inahitaji umakini wa hali ya juu.“kama nilivyoeleza hapo awali kwamba kazi hii itawahusu watumishi wa umma wote, ni dhahiri kwamba  mtakutana na watu wa kada, taaluma,uelewa na matarajio tofauti ambapo mtalazimika kutumia weledi wenu wa mahusiano na mawasiliano (interpersonal and communication skills) katika kufanikisha kazi hii kwa ufasaha,” Dkt. Ndumbaro alisisitiza.

Amewataka washiriki kuwa wasikivu na wepesi wa kuelewa mafunzo haya kwani lengo si kuwapa ujuzi wa kufanya kazi hii peke yake bali kuwajengea uwezo katika kumudu mazoezi kama haya kwa siku za baadae. 

“Nitafurahi endapo miongoni mwenu mtatokea wataalam wa kuendesha zoezi kubwa kama hili siku za usoni kama wataalam waelekezi (Consultants),” Dkt. Ndumbaro aliongeza.

Aidha, amemtaka Mtalaam Mwelekezi kufuatilia kwa karibu utendaji wa kila mshiriki ili kuhakikisha kwamba ameelewa, ameshiriki kikamilifu na kuwa anaweza kuaminiwa siku za baadae kuwa sehemu ya kazi kubwa kama hii. 

Zoezi hili ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Malipo ya Mishahara na Motisha katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2010 ambayo imetokana na juhudi za Serikali za muda mrefu katika kuboresha mishahara na masilahi ya watumishi wa umma. 

Zoezi la Tathmini ya Kazi sio zoezi jipya katika utumishi wa umma kwani zoezi la aina hii lilifanyika mwaka 1998 – 2000 ingawa halikuhusisha utumishi wa umma wote. Zoezi la sasa litapima uzito wa kazi katika utumishi wote wa umma kama ulivyoainishwa katika Hati maalum iliyoanzisha Bodi.Zoezi hili linajumuisha watumishi wa umma katika taaluma mbalimbali kutoka katika maeneo ya pembe zote za Tanzania.

Akitoa maelezo ya awali, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma, Bibi Tamika Mwakahesya alisema katika mwaka 2013/14 Bodi ilifanya utafiti ili kubaini hali ya mishahara na masilahi katika utumishi wa umma.

Katika utafiti huo, ilibainika kuwepo kwa tofauti kubwa sana za mishahara na masilahi katika utumishi wa umma hata kwa kazi zinazofanana. Baada ya utafiti huo ilionekana kuwepo umuhimu wa kuendesha zoezi la Tathmini ya Kazi kama njia ya kubaini uzito wa kazi ambalo maandalizi yake yalianza mwaka 2014/15.

Zoezi hili, tofauti na zoezi lililokuwa limetangulia, linazishirikisha tumishi zote za umma kama zilivyoelezwa kwenye Hati ya kuanzishwa kwa Bodi na limekusudia kujenga uwezo wa watumishi wa umma. 

Bodi itaendesha zoezi hili kwa kumtumia Mtaalam Mwelekezi, ambaye ni Kampuni ya Deloitte Consulting Ltd ambaye ametakiwa kufanya kazi na watumishi 70 kutoka kwenye utumishi wa umma ambao watapatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo, atawasimamia kukusanya na kuchambua taarifa na mwisho kwa wale ambao watakuwa wametimiza wajibu wao ipasavyo, kwa kushirikiana na Bodi, watatunukiwa Hati Maalum za Ushiriki (Certificate of Participation) na kuingizwa kwenye kumbukumbu za Serikali. Zoezi hililinatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 15 kuanzia mwezi Oktaba 2015. 

Comments