Thursday, January 28, 2016

SERIKALI YASEMA HAIJAFUTA VIPINDI VYA BUNGE TBC

NDE4
Waziri wa Habari,Utamaduni, Wasanii,na Michezo  Nape Nnauye akitoa  kauli Bungeni mjini Dodoma Januari 27, 2016.
……………………………………………………………
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Serikali imetolea ufafanuzi kuhusu taarifa za upotoshaji kwa umma kuwa imefuta vipindi vya shughuli za Bunge kuoneshwa katika televisheni ya Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) kama zisemazo taarifa zilizozagaa mitaani.
Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Mose Nnauye wakati akiongea na wananchi moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini kutolea ufafanuzi taarifa za upotoshaji juu ya TBC kufuta vipindi vya matangazo ya vikao vya Bunge.
Mhe.Nape Moses Nnauye amesema Serikali haijafuta vipindi vya Bunge bali ilichofanya ni kubadilisha muda wa kurusha vipindi hivyo kutoka muda wa mchana na kuviweka usiku kwa lengo la kupunguza gharama za kurusha moja kwa moja matangazo hayo ya Bunge na pia  kuwapa fursa wananchi zaidi kuangalia na kufatilia yanayoendelea Bungeni kwa kuwa muda wa usiku watu wengi wanakuwa wamesharejea kutoka katika shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Ameongeza kuwa Serikali imechukua uamuzi wa busara katika hili kwani TBC imekuwa ikitumia Sh Billion 4.2 kwa mwaka kama gharama za urushaji wa moja kwa moja wa matangazo hayo , hivyo itasaidia katika kubana matumizi ya shirika hilo kwani fedha hizo hazipo katika bajeti ipewayo shirika bali ni fedha za ndani zinazokusanywa na shirika hilo
Aidha amesema kuwa sio kitu kigeni kwa Bunge kutotangazwa moja kwa moja kwani kuna baadhi ya mabunge katika nchi nyingine urekodiwa na kurushwa baadae kama kipindi maalum cha Bunge,amezitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni New Zealand, India, Malawi, Lesotho, Uingereza na Singapore.
Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) lilianza kurusha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 ila baada ya Serikali  kukaa na kujadili kwa kina kuhusu gharama za urushaji wa matangazo hayo moja kwa moja ikaamua kubadili mtindo wa urushaji wa matangazo hayo kutoka matangazo ya moja kwa moja kwa siku nzima kwenda kwenye mfumo wa kuyarekodi na kuyarusha katika kipindi cha LEO KATIKA BUNGE.
Post a Comment