Wednesday, January 27, 2016

PINDA MGENI RASMI KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA UTAMADUNI WA WACHINA.

 Mwambata wa Utamaduni katika Ubalozi wa Jamhuri ya watu wa China Bw. Gao Wei akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa mkutano kuelezea maadhimisho ya sherehe za mwaka mpya wa Kichina zitazofanyika Januari 30 mwaka huu jijini Dar es salaam.
Waandishi wa habari na wadau mbalimbali wakifuatilia kwa makini maelezo kutoka kwa Mwambata wa Utamaduni katika Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China Bw. Gao Wei hayupo pichani wakati wa mkutano kuelezea maadhimisho ya sherehe za mwaka mpya wa Kichina zitazofanyika Januari 30 mwaka huu jijini Dar es salaam.PICHA ZOTE NA ALLY  DAUD -MAELEZO.


PINDA MGENI RASMI KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA UTAMADUNI WA WACHINA.
Na Joseph Ishengoma

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda Jumamosi ijayo (30.01.2016) anatarajia kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kusherehekea mwaka mpya wa Kichina.

Mwambata wa utamaduni katika ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Bwana Gao Wei amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya utamaduni wa Wachina nchini.

Maadhimisho ya mwaka mpya wa Kichina ni alama muhimu katika utamaduni wa wachina na uadhimishwa kwa wachina kuungana pamoja na familia zao na kufanya shughuli za kitamaduni ikiwemo michezo.

Bwana Gao Wei amaseme kuwa, maadhimisho ya mwaka huu pamoja na kuwakutanisha jamii ya watu wa China na viongozi mbalimbali wa serikali, yatatoa fursa za kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika, kuendeleza urafiki uliopo na kuhakikisha kila upande unanufaika na urafiki huo.
“Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na watu wake tutaendelea kujenga mazingira rafiki kuhakikisha kila upande unafaidika na urafiki wetu,” amesema.

Bwana Gao Wei ameongeza kuwa moja ya malengo ya maadhimisho hayo hapa nchini ni kutoa ujumbe kuwa jamii ya Watu wenye asili ya China wanakuwa watiifu kwa serikali ya Tanzania na kuleta usawa katika ushirikiano wa kisiasa na biashara.”

Kwa mujibu wa Mwambata huyo, katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja, Dar es Salaam,  kutakuwepo na michezo mbalimbali ya utamaduni zikiwemo nyimbo, muziki, judo, muziki wa ala, na michezo mingine ya kitamaduni.

Aidha Bwana Gao Wei ameeleza kuwa mbali na maadhimisho hayo kufanyika Mnazi mmoja, pia yanatarajiwa kuadhimishwa katika miji mingine ya Arusha, Dodoma na Mwanza katika siku tofauti tofauti.China ilianza kuadhimisha sherehe hizo tangu karne ya 12 ambapo kwa mwaka huu, kilele cha sherehe hizo ni February 8, 2016.

No comments: