Tuesday, January 19, 2016

HISTORIA FUPI YA HAYATI PADRI CALISTI NYAMBO ALIYEFARIKI NCHINI MAREKANI AKIFANYA SHUGHULI ZA UTUME

pd
                                          Hayati Padri Calisti Nauli Nyambo
 Hayati Padre Calisti Nauli Nyambo(pichani) ni mtoto wa tatu wa Familia ya hayati Baba Laurenti Ngasamiaku Nyambo na Mama Augustina Ngambakiha Msaki, alizaliwa tarehe 17/5/1939, katika Kijiji cha Kwamare Kirua Vunjo. Ndugu zake wa kuzaliwa ni Clementina, Martina, Beda, Damas, Adela, Eligi, Flora, Hilda, Domitila na Mary. Calisti alibatizwa na kupokea Sakramenti ya Ekaristi na Kipaimara katika Parokia ya Kirua.  
 ELIMU YA MSINGI
Mwaka 1948 hadi 1953 alisoma katika Shule ya Msingi Iwa hadi darasa la sita. Kwakuwa wakati ule shule ya msingi Iwa ilikua na darasa la kwanza hadi la sita tu, Calisti aliendelea na masomo ya darasa la saba kule milimani Usambara mwaka 1954 katika shule ya Msingi Gare. Mwaka 1955 aliendelea na masome ya darasa la nane katika Shule ya Msingi Kichwele (au Uhuru) katika Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam.  
 ELIMU YA SEKONDARI
Mwaka 1956-1957 Calisti aliendelea na masomo kidato cha kwanza na cha pili katika Shule ya Sekondari Umbwe.Alifuzu vizuri masomo yake akachaguliwa kujiunga na kidato cha tatu na cha nne katika Shule ya Sekondari ya Pugu Dar es Salaam 1958 hadi 1959.
 WITO WA UPADRE
Calisti aliongozwa na Roho Mtakatifu alijisikia kuitwa na kuvutwa na wito wa Upadre. Akaomba kujiunga na masomo ya Seminari kupitia Jimbo Katoliki Moshi. Mwaka 1960 hadi 1962 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho.
Baada ya kuhitimu masomo ya Falsafa, aliamua kukatiza masomo na malezi ya Seminari. Akaajiriwa kufanya kazi Benki na Serikalini. Kutokana na nguvu ya wito wa Upadre fedha za mshahara hazikutosheleza dhamira na malengo ya maisha yake ya kupenda kumtumikia Mungu.  Hivyo aliamua arudi Seminari kuendelea na safari yawito wa Upadre.
Akaomba kujiunga na Jimbo Kuu la Dar-es-Saam. Mwaka 1966 alipelekwa kusoma Teolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala Tabora. Mwaka 1969 alihitimu masomo na malezi ya seminari akapewa Ushemasi na mwaka huo huo tarehe 14 December 1969 akapewa sacramenti ya daraja la upadre na Mwadhama Cardinal Laurian Rugambwa na akawa padre wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
 UTUME WA UPADRE
Kwa muda wa miaka tisa alifanya utume katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Alianza kama paroko msaidizi nabaadaye paroko katika parokia kadhaa za Jimbo Kuu la Dar es salaam. Tangu mwaka 1973 hadi 1976 aliteuliwa na  Mwadhama Kardinali Rugambwa kuwa Vikari  wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam. Kutoka Dar Es Salaam alifanya utume pia katika Jimbo Kuu la Arusha kwa muda mfupi kisha Mhashamu  Askofu Denis wa Jimbo la Arusha akamtuma Marekani kwa masomo ya Chuo Kikuu.
 MASOMO YA CHUO KIKUU
Mwaka 1978 alienda Marekani akasoma katika Chuo cha Majesuiti kilichoko Berkeley, California, akatunukiwa Master Degree ya Teolojia mwaka 1982. Alipenda bado kujiendeleza ndipo alipoenda katika Jiji la Washington DC akasoma katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Amerika (Catholic University of America) na akafuzu vizuri akatunukiwa Master of Arts Degree in Religious Education mwaka 1987.
 UTUME NCHINI MAREKANI
Padre Nyambo alikuwa padre wa kwanza mwafrika kufanya kazi katika jimbo la St. Petersburg, Florida, Amerika. Alianza kwa kufanya utume wakati wa kiangazi (Summer holidays) katika parokia ya Mt. Joseph 1982 na Parokia ya Utatu Mtakatifu (Blessed Trinity) mwaka 1986-1987.
Askofu wa jimbo la St. Petersburg alifurahiwa na kuridhika na maisha na utendaji wa Padre Nyambo ndipo akampa utume kamili kama wakili paroko katika parokia moja katika jiji la Tampa, Florida mwaka 1988-1991. Wakati huo huo alikuwa Mkurugenzi wa jimbo wa utume wa Wakatoliki Waamerika Weusi katika jimbo la St. Petersburg.
 Mwaka 1992-1993 alikuwa Paroko Kiongozi wa parokia ya Mt. Peter Claver Tampa. Kwa kuwa alifanya utume wake vizuri alipewa cheo cha Uparoko tangu mwaka 1993-1997.
 Kwa muda wa miaka sita alikuwa Paroko katika Parokia ya Mt. Joseph St Petersburg, yaani, tangu mwaka 1997 hadi 2003. Mwaka huo huo wa 2003 alikuwa Paroko wa Parokia ya Watakatifu Wote (All Saints Parish) hadi mwaka 2013 alipostaafu kisheria.
 Pamoja na majukumu ya uparoko na ya Kijimbo, Padre Nyambo alikuwa raisi wa utume wa Waamerika Weusi Wakatoliki katika Mkoa wa Florida.  

No comments: