MultiChoice Africa inapenda kuwatangazia wateja wake na watanzania kwa ujumla kuwa Clouds TV sasa imeingia rasmi kwenye DStv.
Kile kilio cha muda mrefu cha watazamaji na wapenzi wa Clouds TV juu ya Clouds TV kukosekana kwenye king'amuzi cha DSTV kimesikika na sasa Clouds TV imeingia rasmi ndani ya DStv.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Uendeshaji MultiChoice Tanzania, Ndugu Ronald Baraka Shelukindo, amesema baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya Clouds TV na Multichoice Africa kuhusu Clouds TV kuingia katika king'amuzi cha DStv, MultiChoice Africa na Clouds TV wamefikia muafaka ambapo watazamaji na wapenzi wa Clouds TV wenye ving'amuzi vya DStv watapata uhondo wa Clouds TV ndani ya DStv.
Akiongezea, Meneja Mauzo wa MultiChoice Tanzania , Ndugu Salum Salum ameelezea furaha ya kampuni yao na akasema, wakati mwingine walikuwa wanashindwa kufikia lengo la kupata wateja wengi zaidi kutokana na kukosekana kwa Clouds TV “hivyo kuanzia sasa, tuna imani kuwa idadi ya wateja itaongezeka maradufu!”.
Clouds TV itaanza kupatikana rasmi ndani ya DStv tarehe 14 Januari 2015, kwenye Chaneli 294, katika vifurushi vyake vyote ikiwemo; Premium, Compact Plus, Compact , Family na kifurushi cha DStv Bomba.
Comments