Monday, October 12, 2015

UBADHIRIFU KIKWAZO CHA USHIRIKA KUSHAMIRI

IMG_6069Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida na Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, (Ushauri na Miradi), Amon Manyama wakipitia makabrasha ya mafunzo ya siku moja juu ya Uimarishaji wa Ushirika wa Akiba na Mikopo kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika (SACCOS na VICOBA) na Maafisa Ushirika wa kutoka Wilaya za Bunda, Bukoba na Sengerema yaliyoandaliwa na ESRF na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo (UNDP) kabla ya kuwasili mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Malaika Beach Resort jijini Mwanza.

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
IMEELEZWA kuwa matatizo ya uendeshaji wa vyama vya ushirika hasa ya kutokuzingatiwa kwa sheria na kanuni za ushirika, wizi na ubadhirifu wa mali yamedhoofisha sana ushirika Mkoani Mwanza.
Hayo yamesema na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Manju Msambya kwenye ufunguzi wa Mafunzo ya Uimarishaji wa Ushirika wa Akiba na Mikopo, Mwanza.
Alisema kutokana na ukweli huo ni vyema vyama vya ushirika vikawa makini katika uchaguzi na kuhakikisha kwamba kila wanapofanya uchaguzi wanachagua viongozi wazuri wenye uchungu na maendeleo ya ushirika na siyo wanaotanguliza maslahi yao binafsi na kupuuza ya wengi.
“Tusaidiane kupambana na maovu na kujenga ushirika ulio imara.” Alisema.
Alisema pamoja na changamoto za kiuongozi Mwanza kwa sasa imepiga hatua kubwa upande wa SACCOS na VICOBA.
IMG_6261Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk.Tausi Kida akifurahi jambo na Mgeni rasmi Mkuu wa wilaya Ilemela, Manju Msambya aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kufungua mafunzo hayo mara tu baada ya kuwasili ukumbini hapo.
“… hatuna budi kuyalinda mafanikio haya kwa uwezo wetu wote. Mafanikio hayo tutayalinda kwa kuhakikisha kuwa SACCOS zinaendeshwa kitaalamu na kwamba sheria na kanuni za ushirika zinazingatiwa ipasavyo.” alisema
Aidha Mkuu huyo wa mkoa, alishukuru ESRF na UNDP kwa kusaidia kugharamia mafunzo kwa watendaji wa SACCOS ili waweze kufanyakazi zao kwa misingi stahiki.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk Tausi Kida alisema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha ushirika wa akiba na mikopo mkoani Mwanza.
Akizungumzia historia ya mradi alisema wao kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) pamoja Tume ya mipango, walianza kutekeleza mradi wa kukuza uchumi, kuleta maendeleo endelevu kupitia utunzaji mazingira, usawa wa kijinsia na kupunguza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi yaani (PEI) toka mwaka 2014.

Post a Comment