Monday, October 12, 2015

CCM ITASHINDA BILA WASIWASI-MHE. MIZENGO PINDA

maguu-620x264MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM),

Mhe. Mizengo Pinda amesema CCM itashinda kiti cha Urais bila wasiwasi
kwa sababu ina mgombea mzuri ambaye hawezi kulinganishwa na wagombea
kutoka vyama vingine.
“Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli ana mvuto
kwa jamii, mtazamo wake wa wapi anataka kuipeleka Tanzania unaeleweka
na uko wazi, katika utumishi wake ana rekodi nzuri, hapendi watu
wavivu sababu yeye ni mchapakazi,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Oktoba 11, 2015) wakati akizungumza
kwa nyakati tofauti na wakazi wa jimbo la Sumbawanga Mjini kwenye
mikutano miwili ya hadhara iliyofanyika katika kijiji cha Mawenzusi,
kata ya Molo na Uwanja wa Stendi ya Chanji uliopo Sumbawanga Mjini.
“Mgombea wetu ni safi sana na hata hao wapinzani wanajua lakini kazi
yao ni kuonyesha kuwa Serikali ya awamu ya nne haijafanya kitu na
kutoa ahadi za uongo kuwa katika siku 100 za mwanzo wataigeuza nchi
iwe kama mbingu. Inawezekana hiyo?” alihoji na kujibiwa na wananchi
kuwa haiwezekani.
Alisema CCM kupitia Ilani yake imetekeleza mambo mengi lakini akakiri
kwamba kazi ya kuleta maendeleo ina changamoto nyingi lakini hazina
budi kupitiwa hatua kwa hatua ili kukabiliana nazo.
Alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM,
Dk. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Bw.
Khalfan Aeshi Hilaly. Pia aliwanadi wagombea udiwani wa kata 19 za
jimbo hilo wakiwemo madiwani wa viti maalum ambao walihudhuria
mikutano hiyo.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kwela, Dkt.
Chrissant Mzindakaya ametangaza rasmi kuwa amemsamehe Bw. Khalfan
Aeshi Hilaly ambaye anagombea ubunge jimbo la Sumbawanga Mjini na
kuahidi kufanya naye kazi kuleta maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya
Sumbawanga na vitongoji vyake.
“Tarehe 21 Agosti mwaka huu nilifanya ibada ya kuadhimisha miaka 75 ya
kuzaliwa kwangu. Nilimwita Bwana Aeshi na kutangaza rasmi kwamba
nimemsamehe na yamekwisha, hakuna haja ya baraza kwani kinachotoa
msamaha ni roho ya mtu binafsi,” alisema.
“Nilitamka Zaburi ya 133 ambayo inasema: Tazama, jinsi ilivyo vema
ndugu wakae pamoja na kwa umoja…. Na hapa namuombea kura kwenu
wana-Sumbawanga na wala msamaha wangu kwa Aeshi usiwe ajenda ya
kisiasa. Mbona Sumaye na Mbowe wanamuombea kura Edward Lowassa wakati
wao walikuwa wanamnanga kila siku?” alisema huku akishangiliwa.
Mei 25, 2014 kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad
Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa iliyofanyika
kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, Dkt. Mzindakaya
alikataa kumsamehe hadharani Bw. Aeshi Hilaly baada ya kupewa fursa ya
kushikana mikono jukwaani na kusameheana.
Mzee Mzindakaya alikataa kufanya hivyo akisema yeye ni mkristu lakini
hakuwa ameandaliwa kiroho kwa ajili ya tukio hilo. “Hapa ni shughuli
ya kanisa na si mkutano wa Chama. Lazima niwe mkweli leo sijajiandaa
kwa jambo hili… Mimi ni mtu mzima, nafsi ya msamaha inahitaji
maandalizi, nahitaji maandalizi ya kiroho,” alisema.
Dkt Mzindakaya ambaye alikumbatiana jukwaani na Bw. Aeshi na kusema
atashirikiana naye kwa lolote kwa sababu ni kijana wake, alitumia
fursa hiyo pia kumuombea kura Dk. Magufuli kwa sababu ni mtu safi na
ni mchapakazi mwenye nia ya kuibadilisha Tanzania kiuchumi kupitia
sekta ya viwanda.
“Miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa inaongoza kwa wingi wa viwanda. Wiki
ijayo Rais Kikwete anaweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha chuma…
hiki kitakuwa kiwanda cha nne kwa ukubwa barani Afrika,” alisema.
Aliwataka Watanzania wawapime wanaowania urais kwa vitendo kwani
baadhi yao miezi kadhaa iliyopita walikuwa wakimsifu Rais Kikwete na
Serikali yake lakini sasa hivi wanamkebehi.
“Rais ni mteule wa Mungu na Ikulu ni mahali patakatifu. Lazima
tupeleke mtu aliye safi, aliyetakata na mwenye mikono safi, na huyo si
mwingine bali ni Dkt. Magufuli,” alisema.
Post a Comment