Halmashauri ya Jiji la Dodoma imesema itafuta umiliki wa viwanja vyote ambavyo havijaendelezwa ndani ya muda uliowekwa kisheria, na kuvitwaa kwa ajili ya kuvigawa au kuviuza kwa wahitaji wengine kwa mujibu wa taratibu za sheria.
Kauli hiyo imetolewa Machi 11, 2026 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Halmashauri hiyo, Ndugu Dennis Godwe, ambaye amesema lengo ni kuwakumbusha wananchi na taasisi zinazomiliki viwanja ndani ya Jiji la Dodoma kutekeleza wajibu wao wa kuendeleza maeneo hayo kwa wakati.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 (Sura ya 113), mmiliki wa kiwanja anatakiwa kukiendeleza ndani ya kipindi kisichozidi miezi 36 tangu tarehe ya kupewa umiliki. Kushindwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa masharti ya umiliki na kunaweza kusababisha kufutwa kwa hati.
Hata hivyo, Halmashauri imebaini kuwapo kwa matukio ya watu wasiokuwa waadilifu kuvamia viwanja ambavyo havijaendelezwa, kuondoa bikoni na kuanza kufanya maendeleo bila kuwa wamiliki halali. Vitendo hivyo vimesababisha migogoro ya ardhi na usumbufu kwa wamiliki halali pamoja na Halmashauri, huku baadhi ya wananchi wakilazimika kufika ofisini kufuatilia maeneo yao yaliyovamiwa.
Aidha, imeonya dhidi ya tabia ya kuanza ujenzi wa kudumu bila kibali cha ujenzi kutoka Halmashauri, ikisisitiza kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria. Ujenzi wowote unaofanywa bila kibali utachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kubomolewa.
Katika kusimamia utekelezaji wa masharti hayo, Halmashauri inaongozwa na Sheria ya Mipangomiji namba 8 ya mwaka 2007, inayosimamia upangaji na maendeleo ya maeneo ya mijini.


No comments:
Post a Comment