Tuesday, March 24, 2015

MWONGOZO WA MHESHIMIWA AL SHAIMAA BUNGENI DHIDI YA ALBINO

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Al Shaimaa Kweigyir, ameitaka serikali kuhakikisha kwamba hukumu za watu wanaokutwa na hatia dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), zinafanyika kwa uwazi, sambamba na kutocheleweshwa ili kulinda roho za Watanzania wanaoendelea kuangamia.
Picha mbalimbali zikimuonyesha mbunge wa Viti Maalumu, Al-Shaymaa Kweigyir, akiomba mwongozo wa Spika bungeni jana mjini Dodoma, kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino). Picha zote na Mpigapicha wetu, Dodoma.
Akiendelea kutoa ya moyoni
Akiendelea kuongea kwa msisitizo juu ya mauaji ya albino Tanzania.

Al-Shaimaa aliyasema hayo bungeni jana akitoa maelezo binafsi kwa kupitia Kanuni ya Kudumu ya Bunge ya (50) 1 inayomtaka mbunge kwa ruhusa ya Spika kutoa maelezo binafsi yanayomhusu au yanayoigusa jamii moja kwa moja.

Mbunge huyo ambaye pia ni mlemavu wa ngozi alisema kwamba endapo hukumu za kesi za wahalifu wa albino zitahukumiwa mapema na kwa uwazi itatoa funzo kwa wengine wanaofikiria kufanya unyama dhidi ya albino hapa nchini.

“Na mimi ni mhanga katika jambo hili kwa sababu watu wanaishi kwa mashaka, hivyo naomba hukumu za wahalifu hao ziwe wazi kila mtu aone ili iwe fundisho kwa waliofanya na wale wanaofikiria siku moja wajiingize kwenye unyama huo.

“Pia naomba sheria za mauaji zirekebishwe ili kulinda haki za walemavu mara baada ya kufanyiwa unyama sambamba na kuwapa adhabu kali wale wote wanaokutwa na hatia dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi,” alisema Kweigyir.

Kweigyir ni miongoni mwa wabunge wanaopigania haki za kuishi za watu wenye ulemavu wa ngozi, likiwa ni janga lililoshika kasi katika maeneo kadhaa ya Tanzania, hususan katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kunakoonekana kushamiri vitendo vya kuwadhuru na kuwaua walemavu hao wa ngozi.

No comments: