WAZIRI PROF. MAGHEMBE AKEMEA MIRADI YA MAJI KUGEUZWA BIASHARA

13
Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, akizungumza na wananchi wa Nyarwana (hawapo pichani) baada ya kuzindua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa kijiji hicho.
   6
Waziri Prof. Maghembe akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili na kuzindua na kuweka jiwe la Msingi kwenye mradi wa Maji wa Nyarwana kabla ya kuzungumza na wananchi.
1
Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe akizungumza jambo na Mhandisi wa Maji wilaya ya Tarime, Vita Mkupa wakati alikagua jenereta la mradi wa Maji wa Nyagisya.
9
Wanafunzi wa shule ya msingi Nyarwana wakimsikiliza Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe (hayupo pichani) wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyarwana.
10
Baadhi ya wananchi wa Nyarwana wakimsikiliza Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe (hayupo pichani)
11
Mwero Kerenge, mzaliwa wa Nyarwanya akimuuliza swali Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe kwenye mkutano wa hadhana baada ya kuzindua na kuweka mawe ya misngi kwenye miradi ya maji.
83
Waziri Prof. Maghembe, akiweka jiwe la msingi la mradi wa Maji wa Nyarwana.
2
Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe, akifungua bomba la maji ya Mradi wa Nyagisya wakati alipokwenda kuzindua mradi huo.
17
Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, akimtwisha maji mwananchi wa Muliba, baada ya kuzindua mradi wa kijiji hicho.
12 
Claudia Luke mkazi wa kijiji cha Nyaryanya akitoa kero yake kwa Waziri wa Maji, Prof. Maghembe.
14
Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe (katikati) akikagua kisima cha Mradi wa Maji Muliba.
15 
Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, akiondoka kwenye jengo la mradi wa Muliba, akiwa na wenyeji wake.
20
Juliana Boke Salima, mkazi wa kijiji cha Muliba, akimuuliza swali Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, katika mkutano uliofanyika kijijini hapo.
…………………………………………………………………………
Hussein Makame-MAELEZO, Tarime
WAZIRI wa Maji Proefesa Jumanne Maghembe amezitaka kamati za maji za vijiji kuacha kuifanya miradi ya maji kama biashara badala yake miradi hiyo iwe huduma kwa wananchi.
Waziri Prof. Maghembe alitoa tamko hilo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi kwenye vijiji vya wilaya mbalimbali za mkoa wa Mara baada ya kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maji.
Alisema miradi ya maji inayozinduliwa kwenye vijiji mbalimbali ni huduma lakini baadhi ya kamati za maji hupandisha bei ya maji kila wiki ili kujikusanyia fedha nyingi za kutekeleza mambo yao.
Hivyo, aliwataka wenyeviti wa kamati hizo kuitisha mikutano na wananchi wa maeneo yao ili kujadili bei ya maji kwa ndoo moja ambayo itakubaliwa na wananchi wote kwa pamoja na kulipwa na wote.
“Mtakapokuwa na kamati ya kusimamia mradi wa maji, kamati ijue kwamba mradi wa maji sio biashara ya maji kwa hiyo hamuwezi kuwa mnapandisha bei ya maji kila siku” alisema Waziri Prof. Maghembe wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyagasense wilaya ya Serengeti na kuongeza kuwa:
“Haiwezekani hata kidogo, ni lazima mkae pamoja na mpange kwamba ndoo moja ya maji mwananchi atachangia shilingi ngapi. Tukichanga fedha kigodo kidogo kwa ajili ya kuweka kwenye mfuko wetu kila unapochota maji na kila mnapoknywesha mifugo, nadhani tutakuwa na uwezo wa kuendesha mradi wetu bila wasiwasi wowote”
Aliwataka wananchi hao kuzingatia kwamba kamati ya maji iwe inafanya kazi kwa niaba ya wananchi na pia iwe inaishirikisha Serikali ya kijiji kwa kila inachofanya na kwamba wakifanya hivyo watajiendesha vizuri.
Akiwa kwenye kijiji cha Muriba wilayani Tarime, Waziri wa Maji Prof. Maghembe alisema wananchi wana haki ya kupata mradi wa maji lakini wanao wajibu kwa kupata haki hiyo.
Alisema ni wajibu wa kila mradi wa maji kuwa na kamati ya maji ya kijiji ambayo itafanyakazi chini ya Serikali ya kijiji na kwamba kila maamuzi wanayoyafanya kuhusu mradi huo wananchi watatakiwa kuyapitisha.
“Kuwa na mradi wa maji kuna wajibu, mradi wa maji ni haki yenu tumejenga uko hapa.Na nyinyi kwa haki hiyo mna wajibu, wajibu wa kwanza ni kuwa na kamati ya kijiji ya maji. Lakini kamati ile iwe inafanya kazi chini ya uongozi wa Serikali ya kijiji, sawa hiyo?”alihoji Waziri Prof. Maghembe na kuongeza kuwa:.
“Sasa hii kamati ikishapanga bei kwamba ndoo moja tutachangia kiasi hiki ili tuweze kulipa umeme, tulipe walinzi, lazima mapendekezo hayo yaletwe kwenye Serikali ya kijiji na baadaye yaletwe kwenye mkutano wa kijiji kama huu hapa ili muyajadili, muyapokee na muyakubali na kuanza kuyafanyia kazi” 
Hivyo alimtaka mwenyekiti wa kijiji cha Muriba na diwani wa kata hiyo kuhakikisha kwamba hata wao walipie bei hiyo ya maji bila kujali vyeo vyao ili wapate fedha za kuendesha mradi huo. 
“Mwenyekiti na wewe mke wako anachota maji, kama ndoo ni shilingi 50 na mke wako alipe 50, mheshimiwa diwani na wewe mke wako anachota maji, usimpige makofi sasa hivi atarudi mapema lakini naye alipe shilingi 50” alisema Prof. Maghembe, Waziri wa Maji.
Waziri Prof. Maghembe alilazimika kutoa muongozo huo kutokana na taarifa kuwepo kwa baadhi ya kamati za maji za vijiji kutumia miradi hiyo kama biashara ili kutunishia mifuko ya vijiji kupata fedha za kutekelezea shughuli nyingine za kijiji.
Upatikanaji wa maji katika vijiji vya mkoa wa Mara unaelezwa kuwa mdogo hata hivyo baadhi ya vijiji vimefanikiwa kupata maji kwa asilimia 100 baada ya kuzinduliwa kwa miradi ya maji ya vijiji hivyo.
Uzinduzi wa miradi ya maji na kuiwekea mawe ya msingi, zilikuwa ni baadhi ya kazi zilizofanywa na Waziri Prof. Maghembe na baadhi ya viongozi wa mkoa huo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji Kitaifa ambayo ilihitimishwa Machi 22, mkoani Mara kwa Kaulimbiu isemayo “Maji kwa Maendeleo Endelevu”.

Comments