






……………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda amewataka wakazi kwenye mikondo ya maji wahame haraka kwa usalama wa maisha yao na si kusubiri waondolewe kwa nguvu.
Mwenda alisema tayari baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walishalipwa fidia na kutafutiwa maeneo mengine na Serikali lakini wamerejea na kuendelea na maisha yao jambo ambalo alisema sasa Manispaa yake haitasita kuwaondoa kwa nguvu.
Akizungumza wakati wa ziara yake aliyoifanya katika maeneo ya mabondeni na mikondo ya maji katika Manispaa hiyo Dar es Salaam jana Meya huyo alisema anashangaa kuona watu wanajenga makazi katikati ya mkondo wa maji na kusababisha maji hayo kukosa uelekeo na kuingia kwenye makazi yaw engine hususan kipindi hiki cha mvua ilhali tayari walishaondolewa.
“Mfano watu wa Kinondoni Hananasif na Suna tayari walishapewa fidia na kupewa viwanja, lakini wengi wao wameshauza viwanja hivyo na kurudi tena maeneo hayo. Hii inashangaza sana. Tunafanya hivi kwa faida ya maisha yao hatutaki kuona watu wanakufa yanapotokea mafuriko.” Alisema Meya Mwenda.
Mwenda alifanya ziara hiyo katika Kata za Makurumla, Tandale, Makumbusho na Mwananyamala na kushuhudia baadhi ya wakazi wakiwa wamejenga nyumba zao katikati ya mikondo ya maji na kusababisha maji kukosa uelekeo na kuingia katika makazi ya watu ikiwemo Mtaa wa Kimamba eneo la Daraja la Mwinyi.
Katika hatua nyingine Meya huyo alimwagiza Mhandisi Mkuu wa Manispaa hiyo kuwasiliana na Wahandisi wa kampuni ya ujenzi ya Strabag kupata ufumbuzi wa tatizo la mifumo ya majitaka inayopita kwenye barabara hiyo kutafuta njia ya kupeleka maji hayo ili kuzuia yasiingie katika makazi ya watu hususan katika kipindi hiki cha mvua.
Hata hivyo Meya huyo amesifu jitihada za wataalamu wa Manispaa hiyo kwa kushirikiana na watendaji za kuhakikisha wanasafisha njia za maji ikiwemo mitaro ma mito mbalimbali akitolea mfano Mto Ng’ombe uliopo Mwananyamala Kisiwani ambao awali ulikuwa ukifurika maji na kusababisha mafuriko maeneo mbalimbali ikiwemo Tandale kwa Mtogole kutokana na kujaa taka ukilinganisha na sasa.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda alifanya ziara yake katika maneo mbalimbali ya mabondeni na kwenye mikondo ya maji yaliyopo kwenye Manispaa hiyo Dar es Salaam jana ili kuona athari za mafuriko zilizojitokeza kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jijini kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kuepukana na mafuriko hayo.
No comments:
Post a Comment