Thursday, August 14, 2014

TAASISI YA WATUMISHI HOUSING KUTUMIA BILIONI 400 KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI WA SERIKALI

4.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Watumishi Housing Company, Dkt. Fred Msemwa akitoa mada kuhusu mkopo wa ujenzi wa nyumba bora za kisasa kwa watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakati wa warsha ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari Jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 14, 2014.
3.
Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakifuatia uwasilishaji wa mada kuhusu mkopo wa nyumba bora za watumishi wa umma wakati wa warsha iliyotolewa na Taasisi ya Watumishi wa Housing Company leo Alhamisi Jijini Dar es Salaam.
PICHA NA BENJAMIN SAWE- MAELEZO
………………………………………
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam
TAASISI ya Watumishi Housing Company imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 400 kwa ajili ya ujenzi za watumishi wa Serikali katika mikoa 13 nchini.
Ujenzi wa nyumba hizo unatarajia kuanza mwezi oktoba mwaka huu, ambapo katika awamu ya kwanza, taasisi hiyo imepanga kujenga jumla ya nyumba 2500 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/15 na Mikoa itayonufaika na ujenzi wa nyumba hizo ni Mtwara, Rukwa,Mbeya, Morogoro, Dodoma, Pwani, na Dar es Salaam.
Mikoa mingine ni pamoja na Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Kigoma na Kilimanjaro, na jumla ya nyumba 50,000 zinatarajiwa kujengwa na taasisi hiyo hadi kufikia mwaka 2019. 
Akizungumza katika warsha ya siku moja kwa Watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Fred Msemwa alisema mara baada ya kukamilika nyumba zinatarajia kuuzwa kiasi cha Tsh. Milioni 19 hadi Milioni 119.
Dkt. Msemwa alisema mpaka sasa Ofisi imeanza utaratibu wa kuuza vipande vitavyowekezwa katika ardhi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Pensheni wa mashirika ya Umma (PPF), mfuko wa pensheni wa watumishi wa umma (PSPF), na mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF), 
Mifuko mingine ni pamoja na mfuko wa pensheni wa watumishi wa Serikali za Mitaa ( LAPF), mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF), pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa, ambapo waombaji watapaswa kupitisha maombi yao kupitia kwa waajiri wao.
Aliongeza kuwa tayari ofisi yake imekwishapata maelekezo kutoka katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ambapo moja ya masharti ni pamoja na makato ya riba yasiyozidi aslimia 10, na mtumishi atatakiwa kutumia kipindi cha miaka 5 hadi 25 ili kurejesha mkopo katika taasisi hiyo.
Akifafanua zaidi Dkt. Msemwa alisema Nyumba hizo zitakuwa ni za kisasa zaidi kwani maeneo yote yaliyojengwa nyumba hizo yamepimwa na kutakuwa na miundombinu bora zaidi ikiwemo barabara, maji na umeme, hivyo aliwataka watumishi wa umma kujitokeza kwa wingi ili waweze kujipatia nyumba hizo.
Kwa mujibu wa Dkt. Msemwa mpaka sasa wamepokea jumla ya maombi 500 kutoka kwa watumishi wa Serikali na ofisi yake imeanza mchakato wa kupitia maombi hayo na kuangalia kama wamekamilisha vigezo vya kimsingi ikiwemo masharti ya kuwa mwajiriwa katika sekta ya umma pamoja na kuwa mwanachama wa mfumo wowote wa pansheni.
“Leo hii watumushi wengi wa Serikali wameshindwa kununua nyumba kutoka katika taasisi mbalimbali, utakuta nyumba ya Tsh. Milioni 30,000,000 mtumishi anatakiwa kukatwa asilimia 10 ya mshahara wake ambayo ni Tsh. 3,000,000, hivyo wengi wao wamejikuta wakishindwa” alisema.

No comments: