WASANII KUSHIRIKI TAMASHA LA KWANZA LA KIMATAIFA LA MUZIKI LITAKALOFANYIKA JIJINI CAIRO, MISRI

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote nchini wa sanaa za muziki wa asili na kiutamaduni kuchangamkia fursa ya kushiriki tamasha la kimataifa la muziki linalotarajiwa kufanyika katika Jiji la Cairo nchini Misri na linaloandaliwa na taasisi ya EL Fayoum International Festival for Traditional Music and Culture. 
Kwa mujibu wa mwaliko uliopokelewa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na kulifikia BASATA, tamasha hilo la kwanza na la aina yake linatarajiwa kufanyika Desemba 17-23, 2014 ambapo wasanii mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali duniani watashiriki. 
Mwaliko huo unasisitiza kwamba washiriki wote wa tamasha hilo watatakiwa kujigharamikia usafiri wa kwenda na kurudi pamoja na Bima. Waandaaji watawajibika kugharamikia usafiri wa ndani, chakula na malazi wakati wote wa tamasha. 
BASATA linahimiza vikundi, vyama, mashirikisho ya Sanaa, wasanii na wadau wa Sanaa kuchangamkia na kutumia fursa hii kujitangaza kwa lengo la kujipatia soko la kimataifa kupitia kuonesha kazi za Sanaa zilizo bora kutoka Tanzania.
Kwa wale wote wanaonuwia kushiriki au kutaka taarifa zaidi kuhusu tamasha hili, Baraza linawaomba wafike katika ofisi zake zilizoko Ilala, Sharif Shamba jijini Dar es Slaam, Idara ya Ukuzaji Sanaa na Masoko au kuwasilina moja kwa moja na baraza kwa barua pepe inayoonekana hapo juu. 
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
Katibu Mtendaji (K)

Comments