Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph, akifafanua jambo kwa Diwani wa kata ya Ololosokwani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika lisiolo la kiserikali la RAMAT inayomiliki Redio Loliondo FM, Bw. Yannick Ndoinyo (kushoto) wakati wa ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na UNESCO. Bw. Al Amin aliambatana na wadau wa maendeleo Meneja Mauzo wa Samsung tawi la Tanzania, Bw. Sylvester Nteere (wa pili kushoto) na Mwakilishi wa Ubalozi wa Uswiss nchini, Bw. Erick Kalunga (hayupo pichani). Kulia ni Afisa Miradi kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO, Myoung Su Ko. wengine wakinamama wakikundi cha kimasaia waliofika kupokea ugeni huo.
Na Mwandishi wetu
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni duniani (UNESCO) limezitaka redio za jamii kuendelea kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii hususan ukeketaji kwa akina mama kwa kuelezea athari zitokanazo na ukeketaji ili kuisaidia jamii yenye mila hizo kuachana nazo kabisa.
Hayo yamebainishwa na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph wakati wa ziara ya kutembelea miradi kwenye vijiji vya Ololosokwani wilayani Ngorongoro na kuzitaka redio za kijamii kuwa sehemu ya kutoka elimu ya katiba ili kuiwezesha jamii kufahamu wajibu wao kama raia ili wakati unapofika waweze kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo.
Al Amin alisema kuwa vipindi vya elimu ya Afya na masuala ya kijamii yahusuyo serikali na jamii kwa ujumla yanapaswa kupewa kipaumbele na redio hizi katika masuala ya huduma za kijamii hususan ndoa za utotoni, ukeketaji na ajira za utotoni ili ziweze kukomeshwa katika jamii kwani zinarudisha maendeleo ya mtoto hasa wa kike.
Sehemu maalum ya anayotumia mtoa huduma wa maktaba hiyo inayofadhiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambapo kutokana na shida ya umeme katika eneo hilo Kompyuta hiyo inatumia umeme wa jua (solar).
“Kwa sasa hapa nchini kumekuwa na mjadala wa Katiba Mpya mchakato unaoendeshwa na Bunge la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma. Wananchi wana haki ya kujua kila kinachoendelea, kushiriki katika mijadala mbalimbali itakayosaidia kupanua uelewa wao ili mwisho wa siku wanajamii waweze kuwa na maamuzi sahihi na hilo ndio lengo la redio” alisema Al Amin.
Alisema kuwa japo matangazo yamekuwa ya muda mfupi redio Loliondo imekuwa faraja na imetoa mchango mkubwa katika kusaidia jamii kupata uelewa kwenye masuala mbali mbali ya kijamii hususan wizi wa mifugo na utunzaji wa mazingira ya kiikolojia kwenye maeneo husika kwenye uwanda wa eneo la pori tengefu la Loliondo.
Nae Mkurugenzi wa RAMAT Yannick Ikayo ambayo inaendesha mradi wa redio ya kijamii ya Loliondo FM alisema kuwa redio hiyo imekuwa mkombozi kwa kutoa elimu kwa jamii na imesaidia kuongeza uelewa na madhara mbali mbali kwenye masuala ya kijamii hususan ukeketaji na utunzaji wa mazingira ya kijamii.
Jengo la Maktaba inayofadhiliwa na UNESCO iliyopo kwenye kijiji cha Ololosokwani wilayani Ngorongoro kwa uangalizi wa Shirika lisiolo la kiserikali la RAMAT.
Loliondo FM Redio ilianzishwa mwaka Oktoba 2013 pamoja na Maktaba na Ujenzi wa Kituo cha Utamaduni ambavyo lengo ni kusogeza elimu kwa jamii ya kifugaji na kupata uelewa wa masuala mbali mbali yanayowazunguka ikiwemo utunzaji wa mazingira.
“Migogoro ya kijamii imekuwa ikipatiwa ufumbuzi hali inayoifanya jamii ya kifugaji kufaidika na redio hii kwani imekuwa na msaada mkubwa kwa jamii yetu na wilaya kwa ujumla hivyo tunaiomba jamii kuipa ushirikiano na kuamini kuwa redio hiyo ni mkombozi wao na kiunganishi kati yao na watawala”, amehitimisha Ikayo.
Wilaya ya Ngorongoro imeonekana kuwa na changamoto katika elimu hasa vijana wa kike kuacha masomo kwa ajili ya kuolewa na wengine kukimbia kukeketwa hali inayohitaji serikali kutoa elimu kubwa kwa jamii ya kifugaji kuachana na mila potofu ikiwemo ukeketaji ulioshamiri.
Wanahabari walitembelea wilayani humo waliwashudiwa wasichana kutoka kabila la kifugaji wakiwa tayari wamekeketwa kwa kuvalishwa mavazi maalum yanaonyesha kutoka kwenye tohara huku wakimshuhudia msichana aliyeshindwa kwenda kujiunga na kidato cha kwanza akiuza mkaa kwa kisingizio cha kukosa ada.
Mkurugenzi wa Shirika lisiolo la kiserikali la RAMAT inayomiliki Redio Loliondo FM, Bw. Yannick Ndoinyo (wa pili kushoto) akielezea maendeleo ya miradi mbalimbali inayosimamiwa na Shirika lake ikiwa chini ya ufadhili wa UNESCO kwa ugeni ulioambatana na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph (katikati) wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo.
Comments