Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Stephen Wasira (katikati) alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jana mjini Dodoma juu ya mkutano wa 30 utakaofanyika nchini mwishoni wiki hii. Kushoto ni Rais wa Benki ya Maendeleo ya Kusini na Mashariki ya Afrika (PTA), Admassu Tadesse na kulia ni Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Kusini na Mashariki ya Afrika (PTA), Admassu Tadesse (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuhusu mkutano wa miaka 30 ya wanahisa na magavana utakao shirikisha nchi 18 za Afrika, mkutano huo utafanyika kesho jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Steven Wasira akifuatiwa na Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Stephen Wasira (kushoto) abibadilishana mawazo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Kusini na Mashariki ya Afrika (PTA), Admassu Tadesse mara baada ya mkutano na waandishi wa habari jana mjini Dodoma. Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile.
Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
19/082014
Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (PTA) itakuwa mkutano wa mwaka utakaofanyikia nchini jijini Dar es salaam tarehe 22 mwezi huu.
Hayo yamebainishwa jana mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Stephen Wasira alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya mkutano huo utakaofanyika mwishoni wiki hii.
“Huu ni mkutano wa kawaida wa mwaka wa Bodi ya Magavana wa nchi wanachama pamoja na Mawaziri wa Fedha, Tanzania ni mwanachama ndio maana mkutano wa 30 unafanyika hapa” alisema Wasira.
Wasira amesema kuwa katika mkutano huo mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo masuala ya fedha na uchumi, maendeleo ya benki ya PTA na mafanikio yake kwa nchi washirika.
Vile vile Wasira amesema kuwa PTA ni benki ya Kiafrika na inafanyakazi nzuri ambapo inaonesha inakua kwa zaidi ya asilimia 30 kwa mwaka kwa miaka kadhaa hadi sasa na imekuwa na mizania ya Dola za Kimarekani mil. 2.8 ikiwa miongoni mwa benki za maendeleo zinazofanya vizuri katika bara la Afrika.
Aidha, Wasira ameongeza kuwa mkutano huo utatanguliwa na semina ya wafanyabiashara itakayofanyika Agosti 21 siku moja kabla ya mkutano mkuu wa Magavana hao ambapo Serikali itawakilishwa na Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba.
Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa benki ya PTA Admassu Tadesse amesema kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele na ni mwanachama hai ambapo imekuwa mfano mzuri kwa nchi wanachama kwa kutoa michango mbalimbali kwa wakati.
Zaidi ya hayo, Tadesse amesema kuwa benki hiyo mwaka huu inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu ili washerehekee na Watanzania.
Tadesse amesisitiza kuwa Benki ya PTA inatoa huduma zake kwa nchi wanachama ikiwa na lengo la kuwa tasisi ya kifedha inayoongoza Mashariki na Kusini mwa Afrika katika utoaji wa huduma za kibenki.
Benki ya PTA ilianzishwa mwaka 1985 ambapo hadi sasa ina jumla ya wanachama 22 ikiwemo nchi 18 ambazo ni Burundi, Comoros, Djibouti Congo, Kenya na Malawi.
Nchi nyinine ni Misri, Eritrea, Ethiopia, Mauritania, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan, Uganda, Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania
Aidha, PTA inashirikiana na nchi nyingine nje ya bara la Afrika ambazo ni Belarus na China.
Washirika wengine ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Kampuni ya Bima ya Mauritia iitwayo Eagle na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Mauritius.
Mkutano wa mwaka huu unafanyikia Tanzania ikiwa ni utaratibu wa benkiya PTA kufanya mikutano ya mwaka kwa mzunguko ambapo washiriki watakuwa Mawaziri wa Fedha, Magavana wa nchi wanachama, sekta binafsi, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali nchini na Wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa.
Comments