Monday, August 25, 2014

AJIRA ZA MADIMBA NI ZA WATANZANIA- MASWI

1[1]
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi akikagua
maendeleo  kinapojengwa Kituo kikubwa cha Kuchakata gesi  eneo la
Madimba mkoani Mtwara. Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Meneja Mradi wa
Ujenzi wa Bomba la Gesi Mhandisi Kapuulya Musumba kutoka Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
2[1]
Mafundi wazawa wakiendelea na shughuli za ujenzi katika eneo
panapojengwa kituo cha kuchakata gesi Madimba. Pichani mafundi
wakishindilia mchanga kwa ajili ya kusawazisha eneo ambapo itafungwa
mitambo mbalimbali katika eneo hilo.
3[1]
Pichani ni baadhi ya nyumba ambazo tayari zimekamilika zitakazotumiwa
na watumishi watakaofanya kazi katika kituo cha Kukachakata gesi
Madimba. Kwa mujibu wa Katibu  Mkuu Wizara ya Nishati na Madini,
Elikim Maswi, amesisitiza kuwa, shughuli mbalimbali katika kituo hicho
zitafanywa kwa kiasi kikubwa na Wataalamu watanzania.
4[1]
Mafundi wakiziba mabomba ya gesi kabla hayajafukiwa ardhini  kwa ajili
ya kusafirisha gesi katika eneo la Msijute Mtwara. Kwa mujibu wa
Mhandisi Kapuulya Musomba, kabla ya mabomba ya gesi hayajafukiwa
ardhini hufanyiwa ‘testing’ kasha sehemu zenye dosari huzibwa kabla ya
kufukiwa ardhini.
Na Asteria Muhozya, Mtwara
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imedhamiria kukifanya kituo unapojengwa mtambo wa kuchakata gesi cha Madimba kuendeshwa na wataalamu wa kitanzania kwa asilimia kubwa.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kueleza kuwa, amefurahishwa na kasi ya ujenzi wa kituo hicho jambo ambalo linaashiria mradi kukamilika katika muda uliopangwa.
Ameongeza kuwa, dhamira ya Wizara na Serikali ni kuhakikisha kuwa, wataalamu wazawa wa kitanzania wanapata ajira katika kila idara itakayohusika na shughuli za uchakataji gesi katika kituo hicho.
“Nataka niseme ajira za Madimba ni za watanzania. Wizara na Serikali inataka wataalamu wa kitanzania kufanya kazi katika kituo hiki, hilo liko wazi, wataalamu watanzania wapo na wanaweza,” amesisitiza Maswi.
Aliongeza kuwa, ili kuhakikisha kwamba watanzania wanapata ujuzi wa shughuli za gesi nchini, serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imekuwa ikiwatumia wataalamu wake kutoka hatua za mwanzo wa ujenzi wa mradi ili waweze kuendeleza shughuli hizo hata baada ya wakandarasi na wataalam kutoka makampuni mbalimbali yanayofanya shughuli za ujenzi wa miundombinu ya mradi huo kuondoka.
Aidha, Maswi amesisitiza kuwa, serikali imejipanga kuhakikisha kwamba kupitia sekta ya gesi na mafuta nchini Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na kuongeza kuwa, jambo hilo linawezekana.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba ameeleza kuwa, kiasi cha gesi kitakachozalishwa nchini kutaliweka vizuri Shirika la Umeme Tanzania kuwa katika hali nzuri ya kuzalisha umeme kutokana na Tanzania kuwa na kiasi kikubwa cha gesi kilichovumbuliwa.
“Gesi tunayo nyingi sana, mnazi gesi imekaa tangu mwaka 1985 haijachimbwa, uhakika wa nishati kwa Tanzania upo”, amesisitiza Musomba.
Ameongeza kuwa, TPDC imefurahishwa na ushirikiano mzuri kutoka serikalini na kutoka Wizara ya Nishati na Madini ambao kwa kiasi kikubwa umewezesha mradi huo kufika katika hatua hiyo kubwa.
“Mwanzo ulikuwa mgumu lakini sasa tuko vizuri sana tunakwenda kama tulivyopanga. Bila msaada wa Wizara na Serikali tusingefika huku. Namshukuru sana Katibu Mkuu kwa kulifanikisha hili,” ameongeza Musomba.

No comments: