Na Magreth Kinabo, Dodoma
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta ameunda kamati ndogo yenye ujumbe wa watu 10 kwa ajili ya kushughulikia masuala ambayo hayakufikia muafaka wakati wa majadiliano ya kupitia sura mbalimbali za Rasimu ya Katiba Mpya kwenye Kamati 12 za Bunge hilo.
Kamati hiyo itakuwa inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Samia Suluhu Hassan,ambapo wajumbe wa kamati hiyo wametoka kila pande ya Muungano yaani watano wametoka Tanzania Bara na watano kutoka Zanzibar.
Aidha Mhe. Sitta akizungumzia kuhusu maendeleo ya kazi za Kamati hizo, ambapo alisema zinaendele vizuri, hivyo kuanzia wiki ijayo sura zote 15 zitakuwa zimepigiwa kura,hivyo Kamati hizo zitakuwa zimemaliza sura 17 ya rasimu hiyo na za nyongeza ifikapo Agosti 27,mwaka huu ili kuanza kuwasilisha katika Bunge hilo kuanzia Septemba 2,mwaka huu.
Hayo yalisemwa leo na Mhe. Samuel Sitta wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokutana nao leo kuhusu muhtasari wa kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo kilichokaa leo kutathmini kazi za Kamati 12 za Bunge hilo lilipofikia pamoja kuridhia baadhi ya mapendekezo ya kuongeza Ibara na sura ndani Rasimu ya Katiba katika Kamati zao.
Mwenyekiti huyo aliyataja mambo ambayo yatashughulikiwa na kamati hiyo, ni muundo wa Bunge katika masuala ya Muungano, uraia pacha, mahakama ya kadhi na kamati ya pamoja ya fedha.
“Haya mambo manne nimeagiza ufanyike utaratibu maalum,” alisema Mhe. Sitta.
Mhe . Sitta akizungumzia kuhusu tathimini ya mwenendo wa Kamati hizo, alisema zipendekeza masuala kadhaa na kuacha mengine kama yalivyo katika rasimu hiyo.
Akizungumzia kuhusu yaliyojadiliwa katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo,kabla ya kukutana na waandishi wa habari, Mhe. Sitta alisema kamati hiyo imepokea mapendekezo kutoka katika kamati mbalimbali kuhusu kuongezeka kwa sura na Ibara za rasimu hiyo.
Aliyataja mapendekezo hayo , likiwemo la Tume ya Marekebisho ya Katiba lililowasilisha na Jaji Warioba kuhusu ardhi, mazingira na rasilimali za taifa, Jumuia ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) na pendekezo la Haki ya Watumiaji huduma na bidhaa ili kuwalinda walaji lililowasilishwa , Hawa Ng’umbi ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo.
Aliyataja mapendekezo mengine ni la Jukumu la Serikali kujenga uchumi imara, ambapo lengo ni kuwa na maendeleo ya uchumi wa ujamaa na kujitegemea na Kuwepo kwa Baraza la Habari, la wajumbe wa 201 kuhusu ardhi, wafugaji, wavuvi pia na wachimbaji wadogo ili ziweze kutungwa Sheria za kusimamia masuala hayo.
Mhe. Sitta alisema kutokana na mapendekezo hayo kutakuwepo na ongezeko la ukurasa na sura kadhaa katika rasimu hiyo.
Alisema Kamati imebaini tatizo la mahudhurio, aliwapongeza wajumbe wa Bunge hilo kutoka upande wa Zanzibar kwa kuwa na mahudhurio mazuri kwenye vikao kuliko kutoka Tanzania Bara kuacha visingizio vya kutohudhuria vikao.
Katika hatua nyingine Mhe. Sitta alisema kutakuwepo na wataalamu kabla ua kumalizika kwa wiki hii kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa kutoka Hazina kwa pande zote za Muungano, ambapo ataukuwepo pia Gavana wa Benki Kuu, Profesa Bonaventure Rutinwa kwa ajili ya suala la uraia pacha, uhamiaji na Profesa Issa Shivji ambaye ataoa ufafanuzi juu ya aina ya Muungano ili kuwa na uwiano kwa kuwa hivi sasa yapo mambo machache.
Comments