Wednesday, October 07, 2015

UNESCO KUENDELEZA UTAMADUNI WA KUZISAIDIA REDIO JAMII

IMG_4940Mkuu wa ofisi na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Utawala na Fedha), Bw. Liberat Mfumukeko alipowasili katika chumba maalum cha wageni kabla ya kuelekea kwenye ufunguzi wa kongamano la siku tatu la Mtandao wa Redio za Jamii katika nchi za Afrika Mashariki (EACOMNET) linalolenga kujadili namna ya kuziwezesha redio hizo kujiendesha katika mipango endelevu kwa kuwa na mipango sahihi ya kifedha bila kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili ili ziweze kutoa mchango unaokusudiwa kwa wananchi linaloendelea katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha.
(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
…………………………………………………
Na Modewjiblog team, Arusha
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), limeonyesha nia yake ya kuendeleza utamaduni wa kuzisaidia redio za jamii nchini Tanzania kwa lengo la kuwawezesha Watanzania walio wengi kupata elimu na hatimae kujinasua katika umaskini.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la Mtandao wa Redio za Jamii katika nchi za Afrika Mashariki (EACOMNET) linalofanyika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) mjini Arusha, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi mkazi wa UNESCO Zulmira Rodrigues alisema kwamba watu zaidi ya milioni 16 wengi wao wakiwa pembezoni mwa Tanzania wanategemea redio za jamii katika kuelimishwa masuala mbalimbali ya ustawi wa jamii jambo ambalo shirika lake linawajibika kwa redio hizo kwa kutoa misaada mbalimbali ili ziweze kujitegemea na kutoa huduma zake kikamilifu.
Alisema anaamini kwamba kwa miaka kadhaa ijayo redio za jamii zitakuwa chanzo cha maarifa kwa watu wengi nchini Tanzania kutokana na uasilia wake na kwa kuyatumikia maeneo ambayo kimawasiliano ni vigumu kufikika, na wakati huo huo vyombo vikuu vya mawasiliano kushindwa kukidhi mahitaji ya wanajamii jambo linalosababisha ukosefu wa kupata habari muhimu na kuzorotesha maendeleo katika jamii husika.
IMG_4942Naibu Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Utawala na Fedha), Bw. Liberat Mfumukeko akisalimiana na Mwenyekiti wa Radio za Jamii kutoka UNESCO India, Prof. Vinod Pavarala katika chumba maalum cha wageni katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha.
Zulmira amezihimiza redio hizo kutoa huduma zinazostahili kwa jamii za kupasha, kuelimisha na kuburudisha, pamoja na kujiwekea mikakati wa kudumu ya kuhamasisha rasilimali fedha zitakazosaidia kuboresha huduma za redio na kuboresha mfumo wa mawasiliano kati kituo cha redio na wanajamii.
Miongoni mwa maboresho yatakayoendelezwa na Unesco ni kusaidia uhakiki wa ubora wa matangazo, vipindi vyenye kuzingatia maadili na ushirikishwaji wa makundi yote wakiwemo wanawake ,vijana ,watu wenye ulemavu na Albinism katika mchakato wa demokrasia, amani na maendeleo .
Kongamano hilo la siku tatu pamoja na mambo mengine linalenga kujadili namna ya kuziwezesha redio hizo kujiendesha katika mipango endelevu kwa kuwa na mipango sahihi ya kifedha bila kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili ili ziweze kutoa mchango unaokusudiwa kwa wananchi.
Kwa niaba ya mtandao wa redio jamii ukanda wa Afrika Mashariki, mwenyekiti wa Mtandao wa redio za Jamii Tanzania, COMNETA Joseph Sekiku aliishukuru Unesco kwa kuziwezesha redio za jamii kutoka nchi za Afrika Mashariki kukutana kwa lengo kushirikiana na kupeana maarifa kuhusu uendeshaji wa redio hizo na zitakavyoweza kutekeleza kwa ubora malengo 17 ya dunia ya maendeleo endelevu na UNESCO India kwa kuleta maarifa mapya kuhusu uendeshaji wa redio za jamii.

No comments: