Thursday, September 10, 2015

NITAHAMASISHA UWEKEZAJI ZAIDI MUHEZA-BALOZI ADADI

Na Mwandishi Wetu, Muheza
Mgombea Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapiduzi (CCM), katika jimbo la Muheza mkoani Tanga, Balozi Adadi Rajabu (Kulia akipokea fomu), amesema atapigana kufa na kupona kuingiza wawekezaji wilayani humo katika nyanja ya kilimo na utalii.

Akizungumza baada ya kunadiwa na mgombea urais wa CCM, John Pombe Magufuli, Adadi amesema mjini hapa jana kwamba ataelekeza nguvu kubwa katika kuvutia wawekezaji ili kuiinua Muheza kiuchumi.

Magufuli, aliyemnadi Adadi kwa kumuita “tunu ya Wanamuheza”, alisema akichaguliwa na kuungwa mkono  Adadi ni mtu mwenye hazina ya  uzoefu adimu na mwenye kuaminiwa na watu na taasisi nyingi ndani na nje ya Tanzania.  Kwa safi hizo ahadi zake ni rahisi kutekelezeka na kuinua   maisha ya wananchi wa Muheza..

Adadi akieleza vipaumbele vyake na mkakati wake wa kuboresha maisha ya watu kiuchumi na kijamii,  aliahidi kupigania kukuza fursa za utalii na kuwepo kwa  viwanda vya kusindika muhogo na matunda, mazao yanayopatikana kwa wingi Muheza.

 Adadi,  ambaye ni mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai mstaafu na balozi mstaafu, alitaja vivutio vya utalii kuwa misitu na viumbehai katika milima ya Amani, na kuongeza kwamba atapigania uimarishaji wa barabara kutoka Pangani hadi Muheza.

Amesema machungwa yanazalishwa kwa wingi Muheza na mengi uharibika kwa kukosa soko la ndani na nje. “Hili lazima tulifanyie kazi,” aliahidi, na kuwataka wananchi wachape kazi kwani viwanda na masoko hudumu kwa kupokea mahitaji yasiyokatizwa kwa msimu mzima.

Muhogo na mtama ni mazao ya chakula ambayo Umoja wa Mataifa unahimiza yalimwe kwa wingi na kusindikwa ili kupambana na tatizo la njaa barani Afrika.

 Adadi amewasihi wananchi wa Muheza kuilinda amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kwani pasipo amani hata uchaguzi wenyewe unaweza kuingia dosari.

Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika tarehe 25 Octoba mwaka 2015
Post a Comment