Wednesday, May 13, 2026

KASI YA UJENZI WA RELI YA SGR IMEONGEZEKA – PROF. MBARAWA

 

Wahudumu wa ndani (Train crew) wa shirika la reli Tanzania (TRC) upande wa Standard Gauge Railway (SGR) wamehudhuria Bungeni Jijini Dodoma kwa mwaliko maalum wa Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ili kuweza kushuhudia uwasilishwaji wa hotuba ya bajeti ya Uchukuzi ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.









Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa amesema Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania inaendelea kuandika historia mpya katika sekta ya usafiri wa reli nchini kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), ambao umeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika vipande mbalimbali vya ujenzi.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Mei 13, 2026, Profesa Mbarawa amesema Serikali imeongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati ambao unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya miundombinu barani Afrika.

Amesema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, vipande vya kwanza vya reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro pamoja na kutoka Morogoro hadi Makutupora vimekamilika kwa kiwango kikubwa na tayari huduma za usafiri zimeanza kutolewa kwa wananchi kupitia vipande hivyo.

Hatua hiyo imeendelea kutoa matumaini makubwa kwa wananchi na wadau wa maendeleo kutokana na mchango wa reli hiyo katika kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kupunguza gharama za usafiri pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kwa upande wa kipande cha Mwanza hadi Isaka, Profesa Mbarawa amesema ujenzi umefikia asilimia 68.77 huku kazi zikiendelea vizuri na kwa kasi kubwa ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora pamoja na kipande cha nne kutoka Tabora hadi Isaka, ambapo shughuli mbalimbali za ujenzi zinaendelea katika maeneo hayo.

Profesa Mbarawa amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya vipande vya mradi huo na kusababisha kuchelewa kwa utekelezaji katika hatua za awali, Serikali imefanikiwa kupata suluhisho la kudumu baada ya kupata mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.277, sawa na takribani Shilingi trilioni 3.32.

Amesema hatua hiyo inaonesha dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha miundombinu ya reli nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi wa usafiri, kukuza biashara na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Katika tukio hilo, wahudumu wa ndani wa treni (Train Crew) wa Shirika la Reli Tanzania upande wa SGR walihudhuria kikao hicho cha Bunge kwa mwaliko maalum wa Waziri wa Uchukuzi ili kushuhudia uwasilishwaji wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, jambo lililoonesha heshima na kutambua mchango wao katika mafanikio ya sekta ya reli nchini.

Mradi wa SGR unaendelea kuwa alama ya mapinduzi makubwa ya miundombinu nchini Tanzania, huku ukitajwa kuwa chachu muhimu ya maendeleo ya uchumi, biashara na usafiri wa kisasa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

No comments:

KASI YA UJENZI WA RELI YA SGR IMEONGEZEKA – PROF. MBARAWA

  Wahudumu wa ndani (Train crew) wa shirika la reli Tanzania (TRC) upande wa Standard Gauge Railway (SGR) wamehudhuria Bungeni Jijini Dodoma...