Friday, September 04, 2015

MAALIM SEIF AREJESHA FOMU


 Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi fomu ya kugombea Urais wa Zanzibar kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bw. Jesha Salim Jecha huko hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bw. Jesha Salim Jecha akionesha fomu za kugombea Urais wa Zanzibar, baada ya kukabidhiwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, huko hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad (OMKR)
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, leo amerejesha fomu ya kugombea Urais wa Zanzibar katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Maalim Seif amerejesha fomu hizo majira ya saa nne asubuhi katika ofisi za tume hiyo zilizoko Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar, baada ya kukamilisha masharti yaliyowekwa na Tume hiyo.

Miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na kula kiapo mahakamani pamoja kuambatanisha shilingi milioni mbili, mambo ambayo ametayatekeleza.
Baada ya kukabidhi fomu hizo kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Bw. Jecha Salim Jecha, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameitaka tume hizo kufanya kazi kwa uhuru na uadilifu.
Amesema kufanya hivyo kutapelekea kufanyika kwa uchaguzi wa amani, huru na wa haki, jambo ambalo litailetea sifa kubwa Zanzibar katika jamii ya kimataifa.

Katika hafla hiyo, Maalim Seif ameambatana na baadhi ya viongozi wa Chama hicho wakiwemo Mgombea uwakilishi wa Jimbo la Malindi Mhe. Ismail Jussa Ladhu, Mgombea uwakilishi wa Jimbo  la Chukwani Mhe. Mansoor Yussuf Himid na Mratibu wa uchaguzi wa CUF Bw. Muhene Rashid.

No comments: