Wednesday, January 21, 2015

KAMATI YA BUNGE YA MAENDELEO YA JAMII YAFURAHISHWA NA MIRADI YA VIJANA

unnamed (15)Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Siad Mtanda akizungumza na wafanyakazi wa Manispaa ya Temeke kamati hiyo ilitofanya ziara ya kutembelea Vikundi vya Vijana vilivyonufaika na Mkopo kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika manispaa hiyo jana jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe.Maabad S. Hoja na wamwisho kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Bw.P. Kagimbo  
unnamed (11)Mwenyekiti wa Temeke Vijana Saccoss Bw. Swaka Abbas akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya Saccoss yao mbele ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii (hawapo pichani) jana jijini Dar es Salaam. Kamati hiyo ilifanya ziara ya kutembelea niradi ya inayoendeshwa na Vijana kupitia Vikundi vilivyopata mkopo kutoka katika Mfuiko wa Maendeleo ya Vijanaunnamed (12)Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Mhe.Maabad S. Hoja akifafanua jambo wakati wa kikao na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii walipofanya ziara ya kutembelea Vikundi vya Vijana vilivyopata mkopo kutoka Wizara ya Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Bw. P. Kagimbo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia (MB) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Siad Mtanda
…………………………………………………………………………………………..
Na Concilia Niyibitanga
Vijana wanatakiwa kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii kama njia pekee ya kujikwamua na umasikini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Said Mtanda (Mb.) jana wakati kamati hiyo ilipokuwa ikikagua miradi inayoendeshwa na vikundi vya vijana katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke vilivyopata mikopo kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mhe. Mtanda alisema kuwa ajira za maofisini haziwezi kutosheleza kila kijana kutokana na ukweli huo ni wakati wa vijana kupambana na hiyo changamoto kwa njia ya kujiajiri kwa kubuni miradi ya kuwatengenezea kipato hali itakayowakwamua katika umaskini.
“vijana msiogope kuthubutu siyo lazima kuanza na mradi mkubwa anza na huo huo mdogo ipo siku utakuwa mradi mkubwa hata mbuyu ulianza kama mchicha”. Alisema Mhe. Mtanda.
Miradi iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni pamoja na mradi wa kilimo cha matikitimaji, mapesheni na ufugaji kuku unaoendeshwa na Kikundi cha Vijana kijulikanacho kama Sokoine Youth Development kilichopo kata ya Somangila, Kigamboni.
Kikundi kingine kilichokaguliwa ni kikundi cha vijana waliohitimu na walioko vyuo vikuu kijulikanacho kama African Legends kilichopo Kigamboni; kikundi hiki kinachojishughulisha na mgahawa pamoja na maswala ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Aidha, Kamati hiyo ilikagua kikundi cha Vijana cha Waungwana Youth Family kinachojishughulisha na kazi za saluni pamoja na muziki; kikundi hiki kiko katika kata ya Sandali.
Mhe. Mtanda aliwakumbusha vijana umuhimu wa kujiunga katika vikundi vya vijana ili watambulike na wajiunge katika SACCOS za vijana katika Halmashauri wazoishi ili iwe rahisi kukopa katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Juma Nkamia (Mb.) alisema kuwa Wizara imejipanga kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi na imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriamali na stadi za maisha zoezi ambalo ni endelevu kwani hadi sasa wataalamu wanazunguka katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo.
Mhe. Nkamia alisema kuwa Wizara itaendelea kuwezesha vikundi vya vijana ambavyo tayari vina miradi ili iweze kukua zaidi na kuwa miradi mikubwa yenye uwezo wa kutengeneza ajira kwa vijana wengine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SACCOS ya Vijana ya Temeke, Bw Swaka Abbas ambapo ndiko mikopo ya vikundi hivyo ilikopitishiwa aliishukuru Kamati hiyo kwa kuwatembelea na kuwatia moyo. Pia aliishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa ushirikiano wanaoupata katika kazi zao za kutokomeza umaskini.

No comments: