Wednesday, January 21, 2015

VITENDO VINAVYOKWENDA KINYUME NA MAADILI YA KIJAMII VYASHAMIRI MIONGONI MWA VIJANA ZANZIBAR

???????????????????????????????
Na Abdulla Ali Maelezo- Zanzibar
Vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya kijamii vimekuwa vikishamiri kwa kasi miongoni mwa vijana wa Zanzibar licha ya viongozi wa Dini, Wazee na Walimu kuvikemea vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Bi Hindi Hamad Khamis wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Mhe. Jaku Hashim katika mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi ulioanza leo Chukwani Zanzibar.
Amesema kuwa hivi sasa imekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya vijana wa kiume hususan wa Kizaanzibari kutoboa masikio, kusuka nywele na kujipodoa jambo ambalo ni kinyume cha sheria, Silka na Utamaduni wa Mzanzibari.
Mhe Bi Hindi amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kupambana na tatizo la uvunjifu wa Mila, Silka na Desturi ikiwa ni pamoja na kushajihisha kutolewa elimu ya Dini na Malezi, Kulinda na Kuhimiza uendelezaji wa Utamaduni pamoja na kusambaza ustaarabu wa Mzanzibari kwa njia ya Sanaa ya Maonyesho, Semina na Makongamano.
Mhe. Bi Hindi ametanabahisha kuwa ili kuondokana na vitendo hivyo viovu, Serikali inapitia upya sheria zilizopo zinazohusiana na mambo ya Mila, Silka na Desturi kwa lengo la kuzipa nguvu ili kupunguza kasi ya vitendo vinavyoipaka matope Zanzibar ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na uwepo wa utandawazi duniani kote.
Aidha amesema tatizo liliopo sio kutokuwepo kwa sheria bali ni usimamizi wa sheria hizo na kuthibitishwa kwa makosa mbele ya vyombo vya sheria ili kuweza kuchukuliwa hatua zinazofaa.
“Kwa kulipatia ufumbuzi tatizo hili, sisi sote hapa ni viongozi na wananchi kwa ujumla tunatakiwa kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo na kutilia nguvu usimamizi wa sheria tunazozitunga”, alieleza Naibu waziri Bi hindi.
Mhe. Bi Hindi amewataka Viongozi, Walimu, Viongozi wa Dini na Wananchi kwa ujumla kushirikiana pamoja katika kupiga vita vitendo hivyo viovu na kutilia mkazo usimamizi wa sheria ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

No comments: